Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baa la njaa Darfur ni matokeo ya binadamu na ni doa la aibu kwa ubinadamu wetu: OCHA

Edem Wosornu, mkurugenzi wa operesheni na uelimishaji wa OCHA
UN Photo/Eskinder Debebe
Edem Wosornu, mkurugenzi wa operesheni na uelimishaji wa OCHA

Baa la njaa Darfur ni matokeo ya binadamu na ni doa la aibu kwa ubinadamu wetu: OCHA

Amani na Usalama

Siku chache baada ya Kamati ya Tathimini ya Njaa kuhitimisha kwamba hali ya baa la njaa iko katika kambi ya Zamzam, karibu na El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, afisa wa wa ngazi ya juu wa  Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu leo ​​aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwambba kwamba "huu ni mgogoro unaosababishwa na mwanadamu na doa la aibu kwenye dhamiri yetu ya pamoja."

Edem Wosornu, ambaye ni Mkurugenzi wa Uendeshaji na Uelimishaji katika Ofisi ya Kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, amewaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba vifaa vya kuokoa maisha katika Bandari ya Sudan viko tayari kupakiwa na kutumwa Zamzam, ikiwa ni pamoja na dawa muhimu, lishe, vifaa vingine, tembe za kusafisha maji na sabuni, lakini ni muhimu kwamba vibali na uhakikisho wa usalama unaohitajika usicheleweshwe.

Wosornu amesema "Hofu yetu kubwa zaidi ilithibitishwa wiki iliyopita Kamati ya tathimini ya njaa ilihitimisha kuwa hali ya baa la njaa iko katika kambi ya Zamzam, karibu na El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini. Hii ni kambi sawa na ambayo madaktari wasio na mipaka au Médecins Sans Frontières walionya takriban miezi sita iliyopita, ambapo mtoto mmoja alikuwa akifariki kila baada ya saa mbili kutokana na utapiamlo. Kamati hiyo iligundua kuwa hali ya baa la njaa pia kuna uwezekano kuwa iko katika kambi zingine za wakimbizi wa ndani na karibu na viunga vya jiji la El-Fasher.”

Hivyo amesema, “njaa inapotokea, ina maana tumechelewa sana. Ina maana hatukufanya juhudi za kutosha. Ina maana kwamba sisi jumuiya ya kimataifa tumeshindwa.”

Afisa wa WFP Stephen Omollo alitoa taarifa kwa Baraza la  Usalama kwa njia ya video
UN Photo/Eskinder Debebe
Afisa wa WFP Stephen Omollo alitoa taarifa kwa Baraza la Usalama kwa njia ya video

WFP inafanya kila iwezalo kusaidia

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, Stephen Omollo ameripoti kuwa shirika hilo linaongeza kwa kiasi kikubwa operesheni nchini kote, Sudan na WFP itatoa kipaumbele katika kuwafikia watu wanaokabiliwa na kiwango cha dharura na janga la njaa pamoja na wale ambao wamekuwa wakimbizi wa ndani.

Omollo amesema, “Tulitahadharisha kwamba njaa ilikuwa karibu. Tulionya kwamba mashirika ya misaada yalikuwa yanazuiwa kufikia sehemu kubwa za nchi hiyo na msaada wa chakula na vifaa vingine muhimu. Lakini maonyo yetu hayajasikilizwa. Kamati ya Tathimini ya Njaa, FRC, wamehitimisha kuwa kuna baa la njaa katika kambi ya Zamzam, karibu na El Fasher, Kaskazini mwa Darfur.”

Ameliambia Baraza la Usalama kuwa "zaidi ya watu 750,000 kwa sasa wameorodheshwa kuwa katika Daraja la 5 la viwango vya njaa vya IPC wakiwa wanakabiliwa na viwango vya janga vya uhaba wa chakula. Takriban watoto 730,000 wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali mwaka huu, aina inayohatarisha maisha. Hii ni mara ya kwanza kwa Kamati kuthibitisha baa la njaa kwa zaidi ya miaka saba, na ni mara ya tatu tu tangu mfumo wa ufuatiliaji wa kimataifa uzinduliwe miaka 20 iliyopita.”

Watu wanaokimbia ghasia wanapitia Kituo cha muda huko Renk kaskazini mwa Sudan Kusini
© UNHCR/Ala Kheir
Watu wanaokimbia ghasia wanapitia Kituo cha muda huko Renk kaskazini mwa Sudan Kusini

Vita inayoendelea Sudan lazima ikome

Maafisa wote wawili wamerejea kusisitiza kwamba mzozo lazima ukome, na usitishaji mapigano unasalia kuwa suluhisho pekee endelevu ambalo litazuia kuenea zaidi kwa baa la njaa.

Katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama, Balozi wa Sudan Al-Harith Idriss al-Harith Mohamed amesema, "tumesisitiza hapo awali na tumetoa wito kwa Baraza la Usalama kulaani nchi zinazotoa silaha na msaada wa vifaa kwa wapiganaji wa RSF kwa kuwa sehemu ya mzozo huu, ambao utasababisha kuzorota zaidi kwa hali ya kibinadamu.”

Mohamed amesema, "baadhi ya nchi kubwa zimekataa kabisa kujumuisha katika azimio 2736, la kulaani kundi la RSF, na pia tuliziomba kuleta shinikizo kwa kundi hilo ili kuondoa kuzingirwa kwa miji mingine inayozingirwa huko Darfur. Na sasa unakuja na kusema juu ya njaa. Iwapo kutakuwa na njaa ya kiwango cha daraja la tano, au hata la mia la IPC, tuko tayari kushirikiana nanyi na tutafungua njia kwa ajili ya usaidizi wowote wa kibinadamu.”