Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio lapitishwa kwa ajili ya sitisho la mapigano duniani wakati wa Olimpiki 2024

Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, (IOC) Thomas Bach (kwenye mimbari) na Tony Estanguet, Rais wa Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki Paris, Ufaransa mwaka 2024, wakizungumza na wanahabari jijini New York, Marekani kuhusu Azimio la sitisho l…
UN Photo/Eskinder Debebe
Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, (IOC) Thomas Bach (kwenye mimbari) na Tony Estanguet, Rais wa Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki Paris, Ufaransa mwaka 2024, wakizungumza na wanahabari jijini New York, Marekani kuhusu Azimio la sitisho la mapigano wakati wa michezo hiyo.

Azimio lapitishwa kwa ajili ya sitisho la mapigano duniani wakati wa Olimpiki 2024

Utamaduni na Elimu
  • Mapigano  yasitishwe duniani kote kuanzia 26 Julai hadi 8 septemba 2024
  • Rais wa Kamati ya kimataifa ya Olimpiki apongeza
  • Ufaransa muandaaji wa Olimpiki yashukuru nchi zilizounga mkono Azimio

Hii leo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha Azimio la kuweko kwa sitisho la mapigano wakati wa kipindi cha michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto itakayofanyika jijini Paris, Ufaransa mwakani 2024 kuanzia Julai 26 hadi Septemba 08, ikijumuisha pia michezo ya Olimpiki ya watu wenye ulemavu.

Azimio hilo namba A/78/L.9 “kujenga dunia yenye amani na bora kupitia michezo na na maadili ya Olimpiki” limepitishwa kwa kura 118 zilizounga mkono, hakuna kura ya kupinga ingawa nchi mbili hazikuonesha msimamo wowote.

Baada ya kura hiyo, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, (IOC) Thomas Bach, amekaribisha kwa moyo mkunjufu na kwa shukrani kubwa kitendo cha kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa kwa azimio hilo. 

Kipindi cha sasa kimefurutu ada kwa mizozo na vita- Bach

“Tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, hatujawahi kuwa na kipindi chenye mizozano, mapigano na vita kama wakati huu. Hili vuguvugu la Olimpiki ni muhimu kuliko wakati wowote ule na kwa hiyo tumefurahishwa mno na uungwaji mkono kutoka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,” ameongeza Bwana Bach.

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ni 193 ilhali waliopitisha ni 118.

Tony Estanguet ambaye ni Rais wa Kamati ya Ufaransa ya kuandaa michezo hiyo amesema wameridhishwa na zaidi ya yote, “tunataka kushukuru kwa dhati nchi ambazo zimeonesha kwa wazi kuunga mkono hii michezo, umuhimu wa hii michezo na nafasi au dhima yake katika jamii kwenye zama hizi.”

Bwana Estanguet amesema anadhani hili ni jambo muhimu kwao kuona idadi kubwa ya nchi zinataka kujihusisha na mafanikio ya michezo na katika kutumia Olimpiki kusongesha utu.

Makubaliano ya sitisho la mapigano yalianza kutumika lini?

Wito huo wa kusitisha mapigano wakati wa michezo ya Olimpiki ulianza kutumika wakati wa michezo ya kale ya Olimpiki huko Olyimpia mwaka 776 Kabla ya Kuzaliwa kwa Kristo.

Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yanalenga kukomesha chuki, na kuruhusu wanariadha, wanamichezo na mashabiki kusafiri na kushiriki salama kwenye mashindano ya Olimpiki.

Makubaliano hayo yalihuishwa mwaka 1992 na sasa yameanza kutumika katika kila michezo ya Olimpiki.

Rasimu ya azimio kwa ajili ya Sitisho la Mapigano wakati wa michezo ya Olimpiki Paris mwaka 2024 iliwasilishwa kwa nchi wanachama na Ufaransa kwa ushirikiano na IOC, IPC na kamati ya maandalizi ya michuano hiyo.