Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Grandi apokea tuzo ya Laurel ya IOC na kutaka watu waige mfano wa timu ya wakimbizi

Paris ni nyumbani kwa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto ya 2024.
© UNHCR
Paris ni nyumbani kwa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto ya 2024.

Grandi apokea tuzo ya Laurel ya IOC na kutaka watu waige mfano wa timu ya wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Michezo ya Olimpiki ikiwa imefunguliwa rasmi hii leo Ijumaa tayari kuanza kesho Jumamosi huko Paris Ufaransa, Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi ameisihi dunia ifuate mfano wa wanamichezo wa timu ya wakimbizi wanaoshiriki michezo hiyo kwa ajili ya kusongesha amani, kuishi kwa pamoja na kuheshimiana.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo Geneva, Uswisi imemnukuu imemnukuu Grandi ambaye pia ni Makamu Mwenyekti wa Mfuko wa Olimpiki kwa wakimbizi akisema michezo ni alama ya matumaini na amani, ambayo amesema kwa bahati mbayá havipatikani kwa kutosheleza duniani hivi sasa.

“Timu ya wakimbizi ni nguzo kwa watu kila mahali. Wanamchezo wanaonesha kile ambacho kinaweza kufanikiwa pindi talanta au kipaji kinapotambuliwa na kuendelezwa na pindi watu wanakuwa na fursa ya kufanya mazoezi na kushindana sambamba na wanamicheoz bora. Hao si kingine zaidi ya kuwa wanajenga hamasa na kuwa mfano kwa wengine,” amesema Grandi ambaye pia leo ameshiriki tukio la kukimbiza mwenge wa Olimpiki akiwakilisha UNHCR na watu milioni 120 waliofurushwa makwao duniani kote.

UNHCR inashirikiana na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, IOC, na Kamati ya Kimataifa kwa ajili ya Olimpiki ya watu wenye ulemavu. IPC sambamba na Mfuko wa Olimpiki kwa wakimbizi kusaidia wakimbizi kwenye michezo hiyo Paris.

Wiki hii Grandi alikuwa mtu wa tatu kupokea tuzo ya Olimpiki ya Laurel, tuzo ya IOC inayotolewa kuenzi mafanikio makubwa kwenye elimu, utamaduni, maendeleo na amani kupitia michezo. Tuzo hiyo ameipokea leo huko Paris.

Timu ya Olimpiki 2024 ya Wakimbizi Paris na Chef de Mission Masomah Ali Zada ​​katika Ukumbi wa Palais des Congrès, Grand Amphithéâtre.
© IOC/Greg Martin
Timu ya Olimpiki 2024 ya Wakimbizi Paris na Chef de Mission Masomah Ali Zada ​​katika Ukumbi wa Palais des Congrès, Grand Amphithéâtre.

Timu ya Olimpiki ya wakimbizi, ROT, huchaguliwa vipi?

Kwa mujibu wa UNHCR, timu hii ya wanariadha 37 kutoka nchi 15 zinazohifahi wakimbizi chini ya Kamati za Kitaifa za Olimpiki. Nchi ihzo ni Austria, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Israel, Italia, Jordan, Kenya, Mexico, Uholanzi, Hispania, , Sweden, Uswisi, Uingereza na Marekani. 

Wanashiriki katika aina 12 za michezo ikiwemo riadha, mpira wa vinyoya, ngumi, baiskeli na kuogelea.

Uteuzi wa wanamichezo ulizingatia vigezo kadhaa na kikubwa kabisa ni uwezo wa kimchezo na wanamichezo wanachaguliwa kupitia program ya IOC ya usaidizi wa mafunzo na masomo kwa wakimbizi.

IOC hushirikiana na kamati za olimpiki za kitaifa kubaini wanamichezo wakimbizi wanaoishi kwenye nchi hizo zinazowahifadhi na ambao wanaweza kukidhi vigezo vya kuwezesha wanamichezo kupata usaidizi wa kuweza kufanya mazoezi, na kuendeleza mustakabali wao.

Kiongozi wa timu hiyo ni Masomah Ali Zada, ambaye alikuwa mmoja wa wanamichezo wa timu ya wakimbizi iliyoshiriki Olimpiki huko Tokyo mwaka 2020 na ndiye muungaji mkono wa juu wa UNHCR.

Kwenye ufunguzi, bendera zitapeperushwa na Cindy Ngamba, raia wa Cameroon aliyepatiwa hifadhi Uingereza na anacheza ngumi na kwa wanaume ni Yahya Al Ghotany anacheza Taekwondo naye anatoka Jordan.

Timu ya kwanza ya wakimbizi ilishiriki michezo ya Olimpiki huko Rio de Janeiro nchini Brazili mwaka 2016 ikiwa na wanariadha 10. Kwa Tokyo walikuwa wanariadha 29 licha ya vikwazo vya coronavirus">COVID-19.