Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yaunda jopo la wataalamu kusaidia Ufaransa tathmini na ukarabati wa Notre Dame

Notre-Dame baada ya moto kuunguza sehemu ya kanisa hilo Aprili 15. (Picha ya Aprili 16 2019)
UNESCO/George Papagiannis
Notre-Dame baada ya moto kuunguza sehemu ya kanisa hilo Aprili 15. (Picha ya Aprili 16 2019)

UNESCO yaunda jopo la wataalamu kusaidia Ufaransa tathmini na ukarabati wa Notre Dame

Utamaduni na Elimu

Kufuatia kuungua kwa  sehemu ya Kanisa Kuu Katoliki la kale, Notre Dame huko Paris nchini Ufaransa hapo jana, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO limeunda kikundi cha wataalamu kwa ajili ya tathmini ya haraka ya uharibifu itakayoanza mapema iwezekanavyo.

Tamko hilo la UNESCO limetolewa mjini Paris, na Mkurugenzi wa kituo cha maeneo ya urithi wa dunia Mechtild Rössler  wakati akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya simu kutoka mjini humo.

UNESCO inashiriki kwenye suala hili kwa kuzingatia kuwa mwaka 1991, kanisa hilo pamoja na maeneo mengine ya ukingo wa mto Seine mjini humo yalitangazwa kuwa maeneo ya urithi wa dunia yaliyoorodheshwa na UNESCO.

Bi. Rossler amesema leo asubuhi askari wazima moto walikuwa wakiendelea kusukuma maji ndani ya jengo ili kuzima moto huo ulioanza jana jioni kwa saa za Ufaransa.

(Sauti ya Mechtild Rossler)

 “Kile tulichoona jana usiku na leo asubuhi ni kwamba takribani theluthi mbili ya paa imeondoka, kwa kiasi imeporomoka au imeungua. Na pengine ndani kuna uharibifu mkubwa wa moto, lakini jengo lenyewe na minara yake mikubwa miwili bado iko imara, na hii ni faida kubwa iwapo unataka kufanya ukarabati au ujenzi mpya”

 UNESCO imesema tathmini itafanywa na mamlaka husika ikiwemo za kitaifa na mitaa, wasimamizi wa eneo hilo na mamlaka za kanisa ili kuandaa mpango wa utekelezaji na kuepusha uharibifu zaidi wa eneo hilo na kuhifadhi vifaa halisi kadri iwezekanavyo.

Kanisa hilo la kale lilijengwa kuanzia kuanzia mwaka 1163 hadi mwaka 1345 na moto wa jana Jumatatu umeteketeza mnara wake mkuu.