Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghana yaripoti maambukizi ya kwanza kabisa yanayoshukiwa kuwa Marburg

Nchini Guinea sasa kumeripotiwa homa ya virusi vya Marburg (Maktaba)
WHO/Junior D. Kannah
Nchini Guinea sasa kumeripotiwa homa ya virusi vya Marburg (Maktaba)

Ghana yaripoti maambukizi ya kwanza kabisa yanayoshukiwa kuwa Marburg

Afya

Ghana imetangaza ugunduzi wa awali wa maambukizi kwa wagonjwa wawili kuwa unaweza kuwa ni ugonjwa wa virusi vya Marburg na ikiwa itathibitishwa, haya yatakuwa maambukizi ya kwanza kurekodiwa nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO Kanda ya Afrika, katika mji mkuu wa nchi hiyo, Accra ikifafanua kuhusu ugonjwa huo imeeleza kuwa Marburg ni homa ya virusi inayoambukiza na ambayo iko katika kundi moja na ugonjwa unaojulikana zaidi wa virusi vya Ebola.   

Uchambuzi wa awali wa sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa wagonjwa wawili chini ya Taasisi ya Ukumbusho wa Noguchi ya Utafiti wa Kimatibabu nchini humo, Noguchi Memorial Institute for Medical Research, umeonesha maambukizi hayo yalikuwa ni Marburg. Hata hivyo, kwa utaratibu wa kawaida, sampuli zimetumwa kwa Institut Pasteur nchini Senegal, ambacho ni Kituo Kishiriki cha WHO kwa uthibitisho.  

Daktari Mark Katz akichukua vipimo kwa mwanamke ambaye alikuwa amekutana na watu wakaribu wa familia yake ambao baadae walifariki kutokana na homa ya Marburg. (MAKTABA)
WHO/Christopher Black
Daktari Mark Katz akichukua vipimo kwa mwanamke ambaye alikuwa amekutana na watu wakaribu wa familia yake ambao baadae walifariki kutokana na homa ya Marburg. (MAKTABA)

Wagonjwa hao wawili kutoka eneo la kusini mwa Ashanti, ambao wote walifariki na hawahusiani, walionesha dalili ikiwa ni pamoja na kuhara, homa, kichefuchefu na kutapika. Walikuwa wamepelekwa katika hospitali ya wilaya katika mkoa wa Ashanti. 

Maandalizi ya uwezekano wa kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa yanaanzishwa haraka huku uchunguzi zaidi ukiendelea. 

"Mamlaka za afya ziko tayari kwenye eneo kuchunguza hali hiyo na kujiandaa kwa mwitikio unaowezekana wa kuzuka kwa ugonjwa. Tunafanya kazi kwa karibu na nchi ili kuongeza ugunduzi, kufuatilia mawasiliano, kuwa tayari kudhibiti kuenea kwa virusi." Ameeleza Dkt. Francis Kasolo, Mwakilishi wa WHO nchini Ghana. 

Ikiwa itathibitishwa, mlipuko huu w ugonjwa nchini Ghana utafanya kuwa mara ya pili kwa Marburg kugunduliwa Afrika Magharibi. Guinea ilithibitisha tukio moja la kwanza katika mlipuko ambao ulitangazwa kuisha tarehe 16 Septemba 2021, wiki tano baada ya kisa cha kwanza kugunduliwa. 

Milipuko ya awali na visa vya hapa na pale vya Marburg barani Afrika vimewahi kuripotiwa nchini Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Kenya, Afrika Kusini na Uganda. 

WHO inaeleza kuwa, "Marburg huambukizwa kwa wanadamu kutoka kwa popo walao matunda na huenea kati ya wanadamu kwa kugusana moja kwa moja na maji ya mwili ya watu walioambukizwa, nyuso na vifaa. Ugonjwa huanza ghafla, na homa kali, maumivu ya kichwa kali na kujisikia vibaya." Wagonjwa wengi hupata dalili kali za kuvuja damu ndani ya siku saba. Viwango vya vifo vya vimetofautiana kutoka asilimia 24 hadi 88 katika milipuko iliyopita kulingana na aina ya virusi na udhibiti wake. 

Ingawa hakuna chanjo au matibabu ya kizuia virusi yaliyoidhinishwa kutibu virusi, uangalizi wa karibu, kurejesha maji mwilini kwa njia ya mdomo au ya mishipa na matibabu ya dalili mahususi, huboresha maisha.