Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni uamuzi mchungu kuamua mkimbizi yupi apewe chakula na yupi akose- WFP

Samberahae, mwenye umri wa miaka 3 na Fedraza mwenye umri wa miaka 2, wakila baada ya kupata mgao wao wa lishe katika Kituo cha Afya cha Msingi cha Ambohimalaza, Ambovombe, Mkoa wa Androy, Kusini mwa Madagascar
© UNICEF/UN0496554/Andriananten
Samberahae, mwenye umri wa miaka 3 na Fedraza mwenye umri wa miaka 2, wakila baada ya kupata mgao wao wa lishe katika Kituo cha Afya cha Msingi cha Ambohimalaza, Ambovombe, Mkoa wa Androy, Kusini mwa Madagascar

Ni uamuzi mchungu kuamua mkimbizi yupi apewe chakula na yupi akose- WFP

Wahamiaji na Wakimbizi

Siku ya wakimbizi duniani ikiwa inaadhimishwa hii leo, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP linaonya ni dhahiri shairi kuwa mgao wa chakula kwa wakimbizi utaendelea kupunguzwa kutokana na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu sambamba na ukata unaozidi kunyemelea shirika hilo.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Roma, Italia, makao makuu ya taasisi hiyo, inasema onyo hilo la kusikitisha linakuja wakati tayari shirika hilo limelazimika kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi katika operesheni zake zote.

Maeneo ambako hali si shwari

Mathalani huko Afrika Mashariki, mgao wa chakula umepunguzwa kwa asilimia 50 kwa wakimbizi na hivyo kuacha wakimbizi huko Kenya, Ethiopia, Sudan Kusini na Uganda wakiwa wameathirika zaidi.

Magharibi mwa Afrika ambako uhaba wa fedha ni mkubwa zaidi, na njaa imefikia kiwango cha juu zaidi katika muongo mmoja, WFP imelazimika kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi wanaoishi Burkina Faso, Cameroon, Mali, Mauritania na Niger.

Makato zaidi Tanzania, Msumbiji na Zimbabwe

Katika nchi za kusini mwa Afrika, WFP kwa wastani husaidia wakimbizi 500,000 kila mwaka.

“Licha ya ukarimu mkubwa wa wahisani, rasilimali zimesalia kuwa chache kukidhi mahitaji ya msingi ya kaya za wakimbizi na hivyo makato zaidi ya mgao yanatarajiwa huko Angola, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Congo, Tanzania na Zimbabwe,” imesema taarifa hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa WFP David Beasley amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema, “kadri njaa inashika kasi duniani kuliko kasi ya rasilimali zilizoko kupatia familia zinazohitaji zaidi msaada wa WFP, tunalazimika kufanya maamuzi ya kuvunja moyo, yaani kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi, mgao ambao wanategemea kwa ajili ya uhai wao.”

Bila fedha zaidi wengi watakumbwa na baa la njaa- Beasley

Bwana Beasleay ameonya kuwa iwapo WFP haitapata fedha zaidi kusaidia wakimbizi- moja ya kundi lililo hatarini zaidi na lililosahauliwa, basi wengi wao watakumbwa na baa la njaa na kulazimika hata kulipa kwa kuutmia uhai wao.

Uhaba wa fedha ukiwa ni kikwazo, WFP inalazimika kuweka vipaumbele wakati inatoa msaada wa chakula kuhakikisha kinafikia kwanza familia zilizo hatarini zaidi, “uamuzi ambao ni mchungu na mara nyingi huacha wakimbizi bila msaada wakati ambao msaada wa chakula unamaanisha uhai au kifo.”

Tuwezeshe wakimbizi wajitegemee

Wakati msaada wa haraka unasalia hofu kubwa ya WFP hivi sasa, shirika hilo linasema, “wakati huu kuliko wakati wowote, uwekezaji endelevu kwenye program za kuchochea wakimbizi kujitegemea unasalia jambo muhimu zaidi.

Ni kwa mantiki hiyo WFP inashirikiana na wadau wake kama vile serikali kujenga mazingira ya wakimbizi kuwa na mbinu za kujipatia kipato sambamba na zile za kuwajengea mnepo pindi kuna changamoto kama za sasa.