Baada ya safari ngumu na ya machungu baharini, mkimbizi mrohingya kutoka Myanmar (kulia) ameungana tena na dada yake (katikati) katika jimbo la Aceh nchini Indonesia

Dunia ina wajibu wa kuwasaidia wakimbizi kuanza upya maisha:Guterres

© UNHCR/Jiro Ose
Baada ya safari ngumu na ya machungu baharini, mkimbizi mrohingya kutoka Myanmar (kulia) ameungana tena na dada yake (katikati) katika jimbo la Aceh nchini Indonesia

Dunia ina wajibu wa kuwasaidia wakimbizi kuanza upya maisha:Guterres

Wahamiaji na Wakimbizi

Vita, machafuko na mateso vimewalazimisha zaidi ya watu milioni 80 kote duniani kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao huku wakiacha kila kitu kwa ajili ya kuokoa maisha yao na ya familia zao. 

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa siku ya wakimbizi duniani ambayo inaadhimishwa kila mwaka Juni 20. 
 Katika ujumbe huo Guterres amesema “Wakimbizi lazima waanze upya maisha yao. Lakini kwa wengi wao janga la corona au COVID-19 limepokonya uwezo wao wa kuishi na hivyo kuchochea unyanyapaa, kubaguliwa na kuwaweka katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya gonjwa hilo.” 
 
Ameongeza kuwa wakati huohuo wakimbizi kwa mara nyingine wamedhihirisha mchango wao wa thamani kwa jamii zilizowapokea kama wafanyakazi muhimu na wa msitari wa mbele katika kupambana na janga hilo. 
Bwana Guterres amesisitiza kuwa “Tuna wajibu wa kuwasaidia wakimbizi kujenga upya maisha yao. COVID-19 imetuonyesha kwamba tunaweza kufanikiwa tu endapo tutasimama pamoja. Katika siku hii ya wakimbizi natoa wito kwa jamii na serikali kuwajumuisha wakimbizi katika huduma za afya, elimu na michezo. Tunapona pamoja wakati wote tunapopata huduma tunazozihitaji, tunajifunza pamoja wakato wote tunapopewa fursa za kusoma, na tunshamiri pamoja wakati tunapocheza kama timu na kuheshimiana.” 
  
Katibu Mkuu ameongeza kuwa katika siku hii ya wakimbizi anazipongeza nchi ambazo zimewakirimu wakimbizi. 
 
Lakini amesema “Tunahitaji msaada zaidi kutoka kwa serikali, sekta binafsi, jamii na watu binafsi endapo tunataka kusongambele pamoja kuelekea mustakbali jumuishi ulio huru bila ubaguzi.” 
 
Akitoa mfano Guterres amesema wakimbizi ambao wamekutana nao wamemdhihirishia inamaanisha nini kwao kujenga upya maisha yao huku wakikusanya nguvu ya kuboresha maisha ya wengine walikokaribishwa. 
 
“Kama kamishina mkuu wa wakimbizi kwa miaka 10 nilihamasishwa sana na ujasiri, mnepo na ari ya wakimbizi. Nawashukuru wakimbizi na watu waliotawanywa kote duniani na narejea kusema binabsi nilivyotiwa hamasa kwa yale waliyotufundisha sote kuhusu nguvu ya uponyaji na matumaini. Katika siku hii ya wakimbizi na siku zote, tunasimama pamoja na wakimbizi.”