Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inapotea kwa kujikita katika matumizi ya mafuta kisukuku aonya Guterres 

Nishati  ya kisukuku ni moja ya visababishi vya hewa chafuzi zinazoongeza joto duniani
UN
Nishati ya kisukuku ni moja ya visababishi vya hewa chafuzi zinazoongeza joto duniani

Dunia inapotea kwa kujikita katika matumizi ya mafuta kisukuku aonya Guterres 

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba mwenendo wa sasa wa uchumi wa dunia ambao unajikita zaidi katika matumizi ya rasilimali kama mafuta kisukuku utaongeza zahma ya mfumuko wa bei, changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na vita. 

António Guterres ametoa onyo hilo wakati akihutubia kongamano kubwa la uchumi kuhusu nishati na hali ya hewa mjini Washington DC, nchini Marekani, kongamano lililoitishwa na Mjumbe Mkuu wa Marekani kuhusu mabadiliko ya tabianchi, John Kerry, na mwenyeji wa kongamano hilo Rais Joe Biden wa Marekani. 

Mkutano huo unajumuisha nchi zinazowakilisha asilimia 80 ya pato la dunia GDP, idadi ya watu na uzalishaji wa gesi chafuzi, kulingana na ikulu ya Marekani White House. 

Suluhu isiyo na mwisho 

Suluhu ya ukuaji wa uchumi iko bayana Katibu Mkuu amewaambia wawakilishi katika mkutanmo huo kwamba "Tuna rasilimali zisizo na kikomo katika matumizi yetu linapokuja suala la mahitaji ya nishati. Upepo, jua na mawimbi haviishi kamwe. Iwapo tunaweza kubadilisha kwa ufanisi mafuta yasiyo na kikomo, yanayochafua mazingira na rasilimali zisizo na kikomo jadidifu zinazoweza kutumika tena, tunaweza kuleta uwiano wa nishati na kuufanya uongezeke." 

Nishati ya kisukuku inayochoma hutoa idadi ya vichafuzi vya hewa ambavyo ni hatari kwa mazingira na afya ya umma.
Unsplash/Andreas Felske
Nishati ya kisukuku inayochoma hutoa idadi ya vichafuzi vya hewa ambavyo ni hatari kwa mazingira na afya ya umma.

Ameongeza kuwa bei thabiti na ukuaji endelevu unaweza kufikiwa iwapo vyanzo vya nishati mbadala vitapewa kipaumbele.  

Zaidi ya hayo, amesema husaidia kupunguza utoaji wa hewa ukaa na kusaidia katika usalama wa nishati. 

"Wakati wa kucheza kamari umekwisha. Ulimwengu umecheza kamari kwenye mafuta kisukuku na kupoteza”, ametangaza Bwana. Guterres. 

Soundcloud

Hatari ya wazi na ya sasa 

Hakuna kinachoweza kuwa wazi zaidi kuliko hatari ya upanuzi wa wigo wa matumizi ya mafuta kisukuku leo hii, ameongeza Katibu Mkuu. 

 "Hata kwa muda mfupi, matumizi hayo hayaleti maana ya kisiasa au kiuchumi. Lakini bado tunaonekana kunaswa katika ulimwengu ambao wazalishaji wa mafuta na wafadhili wana ubinadamu tu mambo yanapowafika kooni. Kwa miongo kadhaa, wengi katika tasnia ya mafuta wamewekeza sana katika sayansi ghushi na uhusiano wa umma na hadithi za uwongo ili kupunguza jukumu lao la kuchangia mabadiliko ya tabianchi na kudhoofisha sera muhimu za dhidi ya mabadiliko ya tabianchi." 

Guterres amelinganisha tasnia ya mafuta kisukuku yenye faida kubwa na mbinu za kashfa za tumbaku za katikati ya karne ya 20. 

Lazima kuwajibika 

Katibu mkuu amesisitiza kwamba “kama ilivyo kwa maslahi ya tumbaku, maslahi ya nishati ya mafuta kisukuku na ushirikiano wao wa kifedha haupaswi kukwepa uwajibikaji. Hoja ya kuweka kando hatua za mabadiliko ya tabianchi kushughulikia matatizo ya kitaifa pia haina maana.” 

Amesema uwekezaji wa awali katika nishati jadidifu, ungeepusha hali ya leo kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na ongezeko kubwa na tete la bei ya mafuta na gesi duniani kote. 

Mradi kama huo wa kubadili samadi kuwa nishati unaotekelezwa na FAO nchini Tanzania, kwa upande wa Rwanda tayari umeleta manufaa kwani katika makazi yaliyoboreshwa kuna mfumo wa kukusanya samadi kutoka kwa ng'ombe inatumiwa kama nishati mbadala.
UNEP-UNDP Rwanda/ Jan Rijpma
Mradi kama huo wa kubadili samadi kuwa nishati unaotekelezwa na FAO nchini Tanzania, kwa upande wa Rwanda tayari umeleta manufaa kwani katika makazi yaliyoboreshwa kuna mfumo wa kukusanya samadi kutoka kwa ng'ombe inatumiwa kama nishati mbadala.

Kitendawili cha Ukraine 

"Kwa hivyo, tuhakikishe vita ya Ukraine haitumiwi kuongeza utegemezi huo wa mafuta kisukuku. Matatizo makubwa zaidi ya leo ya ndani kama mfumuko wa bei na bei ya gesi yenyewe tayari ni matatizo ya tabianchi na mafuta.” Ameongeza Guterres. 

Kwa mara ya pili wiki hii katika hafla kubwa ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mkuu amesisitiza mpango wake wa mambo matano wa mapinduzi ya kuingia katika nishati mbadala. 

"Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ndio dharura yetu kubwa kwa sasa", amesema, akizitaka serikali "kukomesha matumizi ya nishati ya mafuta kisukuku. Mapinduzi ya nishati mbadala yanaanza sasa", amehitimisha ujumbe wake Katibu Mkuu.