Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAHAMU: Mambo 5 ya kusaidia jamii kabla, wakati na baada ya dharura

Mgao wa kuku kutoka FAO kwa ajili ya ufugaji kwa wakazi wa  Cabo Delgado nchini Msumbiji waliokumbwa na dharura kufuatia mapigano kwenye eneo hilo.
©FAO/Fábio de Sousa
Mgao wa kuku kutoka FAO kwa ajili ya ufugaji kwa wakazi wa Cabo Delgado nchini Msumbiji waliokumbwa na dharura kufuatia mapigano kwenye eneo hilo.

FAHAMU: Mambo 5 ya kusaidia jamii kabla, wakati na baada ya dharura

Msaada wa Kibinadamu

Majanga, kama vile matetemeko ya ardhi au mapinduzi ya kijeshi vinaweza kutokea ghafla, au ukame na mafuriko hujiimarisha taratibu. Aina hizi za dharura ni changamoto kwa watu kila mahali, lakini kwa wale ambao mbinu zao za kujipatia kipato au chakula zinategemea kilimo au rasilimali asili pekee, majanga haya mara nyingi huwa na madhara makubwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO, linasaidia jamii kushughulikia changamoto hizi kupitia mbinu mbalimbali za kutambua mapema uwezekano wa janga kutokea na hivyo kujenga mbinu za kujiandaa ili jamii ziweze kuwa na mnepo pindi shida inatokea.
Hizi ni njia 5 ambazo kwazo FAO inatumia kusaidia watu kabla, wakati na baada ya dharura kutokea.

1. Hatua za kinga

Majanga mengi, kama vile majanga ya asili kwa kiasi kikubwa hayaepukiki, lakini kuna hatua nyingi zinaweza kuchukuliwa ili kupunguza kiwango cha madhara yanayoweza kutokea.
Mathalani mwezi Julai mwaka 2020, wataalamu walipotabiri hatari ya mafuriko makubwa kwa jamii za wabangladesh kando mwa mto Jamuna, FAO ilishirikiana haraka na wadau kulinda jamii dhidi ya madhara hayo.

FAO ilipatia wanajamii mapipa ya kuhifadhi vyakula, mapipa ambayo yanaelea kwenye mafuriko ambamo humo walihifadhi mbegu, nafaka na vifaa vingine muhimu.
Mafuriko yalipoanza na kisima cha maji kufurika maji machafu, Kokila Akhter alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu na afya yake ilikuwa ni muhimu kuliko kitu chochote. “Nilihifadhi maji safi kwenye pipa, maji kwa ajili ya kupikia na k unywa. Nilikunywa maji safi na kunisaidia kusalia na afya njema wakati wa ujauzito,” anasema Bi. Akhter.

FAO inapatia wakulima nchini SOmalia mafunzo ya kukabiliana na viwavi jeshi ambao huvamia mazao kama haya maharage.
©FAO/Arete/Ismail Taxta
FAO inapatia wakulima nchini SOmalia mafunzo ya kukabiliana na viwavi jeshi ambao huvamia mazao kama haya maharage.

2. Kuwekeza kwenye uchumi wa wenyeji

Mgao wa fedha taslimu, vocha na kazi kwa malipo ni program ambazo huwezesha jamii kuamua kitu gani wanahitaji zaidi na kuamua ni bidhaa au huduma gani anunue kwenye soko lililo Jirani naye. Programu hizi zinaweza kukwamua jamii haraka zaidi kutoka shida ya ukosefu wa chakula, lishe na mbinu ya kujipatia kipato. Ni mkombozi wakati wa majanga.

Mwanamke mmoja kiongozi wa kaya ambaye hivi karibuni alinufaika na usaidizi wa aina hii wa FAO huko Afghanistan anasema program hii ilimnusuru wakati wa janga la COVID-19.
“Tatizo letu ni kwamba hatuwezi kununua chakula au bidhaa nyingine muhimu. Fedha tunazopatiwa na FAO tulitumia kununua mchele na vifaa vya shule kwa ajili ya wajukuu zangu,” alisema mnufaika huyo.

Mwaka 2021 pekee, FAO ilisaidia kaya maskini 200,000 nchini Afghanistan kupitia mgao wa fedha taslimu au miradi ya kazi kwa malipo.

3. Kusaidia mtu ili ajisaidie

Mara nyingi katika majanga au majanga ya asili watu hupoteza maeneo  yao ya ardhi, mifugo, pembejeo za kilimo au mali nyingine na hivyo kufanya vigumu kwa wao kuanza tena maisha na kujipatia kipato baada ya majanga.

Kabla, wakati na baada ya dharura au majanga, FAO husambaza kwa wakulima makasha yenye pembejeo ili waweze kuanza tena kupanda mazao ili wapate chakula na mazao mengine ya kuuza kwa ajili ya kipato.FAO pia husambaza chanjo au huduma nyingine za mifuko ili kulinda mifugo, moja ya sehemu nyingine muhimu kwa jamii kujipatia kipato.

Pindi mafuriko na baa la nzige lilipokumbwa Somalia mwaka jana, FAO iliingilia kati ili wanajamii waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Wakulima kama Iraado Amir Omar siyo tu walinufaika na mgao wa fedha taslimu kutoka FAO kukidhi mahitaij yao ya haraka, bali pia walipatiwa mbegu na vifaa vya kilimo ili kuendeleza kilimo kwa muda mrefu.

“Mbegu zilifika wakati nahitaji zaidi. Sikujitaji fedha kununua mbegu, lakini angalau sasa naweza kupanda mazao,” amesema Iraado.

“Msaada kutoka FAO ni muhimu sana kwa sababu maisha yetu yanategemea ardhi,” amesema jirani yake aitwaye Ali Mahamud Rubaax akiongeza kuwa ,”natumai katika siku zijazo, hizi mbegu nipandazo zitabadili maisha yangu na ya familia yangu.”

4. Kujenga mnepo katika mbinu za kujipatia kipato

Watu wenye uwezo wa kuendeleza njia zao za kujipatia kipato wana uwezo mkubwa wa kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi na majanga kwenye maisha yao.

FAO inafanya kazi na nchi duniani kote kutathmini madhara ya mabadiliko ya tabianchi na kutoa mwongozo kuhusu mbinu za kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi. 

Kwa kutumia mbegu tofauti tofauti, nyavu bora za uvuvi, au mbinu ya mzunguko wa upanzi wa mazao, FAO inasaidia watu kuwa na mbinu za kujipatia kipato zilizo na mnepo sambamba na mustakabali ulio endelevu.

Mfano ni huko Amerika ya Kati kwenye eneo lililo na ukame wa kupindukia, FAO inasaidia familia za wakulima zilizo hatarini kwa kuwapatia mbinu za usimamizi na matumizi bora ya maji.

 

Vita au majanga vinapolazimu rai a kukimbia makwao, FAO inapeleka msaada siyo tu kwa wakimbizi bali pia kwa wenyeji wanaohifadhi
©FAO/Telcínia Nhantumbo
Vita au majanga vinapolazimu rai a kukimbia makwao, FAO inapeleka msaada siyo tu kwa wakimbizi bali pia kwa wenyeji wanaohifadhi

5. Kusaidia jamii za wakimbizi

Familia zilizo hatarini zinalazimika kukimbia makazi yao kutokana na mizozo na majanga, na mara nyingi hupata hifadhi kwenye kambi au kwa wenyeji.

Wakati mwingine, jamii hizi za wenyeji zinakuwa zinahaha kupata rasilimali. Kwa hiyo wageni wakimbizi wanaposaka vyanzo vya kipato na chakula, inaweza kuibua changamoto na jamii wenyeji.
Kusaidia jamii za wenyeji na wakimbizi, FAO inatekeleza miradi ya kuwezesha ongezeko la uzalishaji wa chakula na kuchochea fursa za kiuchumi kwa manufaa ya wote.

Kufuatia ghasia huko Cabo Delgado, nchini Msumbiji, FAO ilisaidia familia za wakimbizi kwa kuzipatia pembejeo, sambamba na kupata mkopo ili ziweze kununua mbegu na mahitaji mengine.
Jamii za wenyejii zinanufaika na msaada kama huo pia ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza uhaba wa rasilimali.

FAO inashirikiana na wadau wakuu kama vile mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia, serikali na wadau wa sekta binafsi ili kushughulikia changamoto nyingi zitokanazo na dharura ili hatimaye jamii ziweze kukabili vyema dharura na ziweze pia kuibuka upya na kwa uimara zaidi sasa na siku za usoni.