Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usawa ndio jawabu mujarabu la kutokomeza VVU na Ukimwi- WHO

Kwenye mji mkuu wa Dd'jamena Chad, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 17 akitabasamu baada ya kupimwa na kubainika kuwa hana VVU.
© UNICEF/Frank Dejong
Kwenye mji mkuu wa Dd'jamena Chad, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 17 akitabasamu baada ya kupimwa na kubainika kuwa hana VVU.

Usawa ndio jawabu mujarabu la kutokomeza VVU na Ukimwi- WHO

Afya

Ikiwa leo ni siku ya Ukimwi duniani maudhui yakiwa kumaliza ukosefu wa usawa ili kila mtu aweze kupata huduma za kujikinga au kupunguza makali dhidi ya Virusi Vya Ukimwi, VVU na Ukimwi, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, kanda ya Afrika limesema maudhui hayo yamekuja wakati muafaka kwa kuwa ukosefu wa usawa ndio chanzo cha kuibuka na kusambaa kwa magonjwa ya milipuko na yaliyojikita mizizi barani Afrika.

 

Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa mshikamano wa kimataifa utasaidia kumaliza ukosefu wa usawa na hivyo kuhakikisha kila mtu anapata haki sawa za kibinadamu katika kujikinga na kutibiwa VVU na Ukimwi.

WHO inasema barani Afrika pekee, watu 1,300 hufariki dunia kila siku kutokana na magonjwa yanayohusiana na VVU na Ukimwi kwa hiyo “lazima tuhakikishe kila mtu, kokote aliko ana fursa sawa ya kinga dhidi ya VVU, kupata vipimo, tiba na huduma za matunzo ikiwemo chanjo pia dhidi ya COVID-19 na huduma nyinginezo muhimu.”

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 67 ya watu wote wanaoishi na VVU wako katika ukanda wa WHO barani Afrika.

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa UN

Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ili kushinda UKIMWI na kujenga ustahimilivu dhidi ya janga la kesho tunahitaji kuchukua hatua sasa akitolea mfano kutumia uongozi ndani ya jamii ili kuleta mabadiliko, kupambana na unyanyapaa, na kuondoa sheria, sera na mazoea ya kibaguzi na ya kuadhibu.

“Ni lazima tuondoe vikwazo vya kifedha kwa huduma ya afya na kuongeza uwekezaji katika huduma muhimu za umma ili tufikie huduma ya afya kwa watu wote kila mahali.Tukifanya hivi itahakikisha upatikanaji sawa wa kinga, upimaji, matibabu na matunzo ya VVU, ikijumuisha chanjo na huduma za COVID-19. Kwa pamoja, tujitoe tena kukomesha ukosefu wa usawa na kukomesha UKIMWI.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na Ukimwi, UNAIDS linasema miaka 40 tangu mgonjwa wa kwanza wa Ukimwi aripotiwe duniani, bado VVU vinatishia ulimwengu.

Na kama hiyo haitoshi leo hii dunia haiko kwenye mwelekeo wa kufanikisha azma yake ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 si kwa sababu ya ukosefu wa ufahamu wa kile cha kufanya,  au ukosefu wa mbinu za kutokomeza UKIMWI, bali kwa sababu ya mifumo ya ukosefu wa usawa ambayo inazuia majawabu dhidi ya kinga na tiba kwa VVU kufikia kila mhitaji.