Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unyanyapaa dhidi ya wanaoishi na VVU tupilia mbali, ongeza ufadhili kwenye huduma

Grace Amodu, alitambua kuwa ana VVU alipokuwa na umri wa miaka 7. Sasa ana watoto wawili na wote hawana maambukizi ya VVU kutokana na huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, PMTCT.
UNAIDS Nigeria
Grace Amodu, alitambua kuwa ana VVU alipokuwa na umri wa miaka 7. Sasa ana watoto wawili na wote hawana maambukizi ya VVU kutokana na huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, PMTCT.

Unyanyapaa dhidi ya wanaoishi na VVU tupilia mbali, ongeza ufadhili kwenye huduma

Afya

Ikiwa leo ni siku ya Ukimwi duniani, ripoti mbalimbali zilizotolewa kuelekea siku hii kuhusu hali ya maambukizi ya Ukimwi duniani zinaonesha pengo kubwa la ukosefu wa usawa kati ya wanaopata huduma na wasiopata huduma na hali ni mbayá zaidi kwa wanawake na watoto. 

Ni kwa kuzingatia ripoti hizo, ile ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la kukabiliana na Ukimwi, UNAIDS, mada yetu kwa kina inaangalia changamoto na harakati za wale ambao wanaishi na Virusi Vya Ukimwi, au VVU za kuhakikisha watu wengine wenye VVU wanapata huduma na hivyo kusaidia kuongeza ustawi wa maisha yao na wakati huo huo kupunguza maambukizi mapya. 

Tunajikita kabisa nchini Nigeria moja ya nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ambako ripoti inasema hali si shwari ya maambukizi. 

Ninaishi na VVU na nafikishia dawa wale wanaokumbwa na unyanyapaa- Grace 

Grace Amodu mchechemuzi wa Chama cha kimataifa cha wanawake wanaoishi na virusi vya Ukimwi, ICW, na  Mfamasia wa kijamii nchini Nigeria, anasema anaishi na virusi vya Ukimwi, VVU.  

Alifahamu kuhusu hali yake ya kuwa na maambukizi ya VVU tangu akiwa na umri wa miaka 7 na tangu wakati huo amekuwa anakunywa dawa.  

Wanachama wa chama cha kimataifa cha wanawake wanaoishi na UKIMWI, ICW nchini Nigeria wakiwa kwenye mkutano wao ambako hupeana matumaini na kujiamini. Kulia ni Assumpta Reginald, Mratibu wa ICW Kanda ya Afrika Magharibi.
UNAIDS Nigeria
Wanachama wa chama cha kimataifa cha wanawake wanaoishi na UKIMWI, ICW nchini Nigeria wakiwa kwenye mkutano wao ambako hupeana matumaini na kujiamini. Kulia ni Assumpta Reginald, Mratibu wa ICW Kanda ya Afrika Magharibi.

Japo ninaishi na VVU watoto wangu nimejifungua hawana maambukizi 

Akiwa ameshikilia simu yake ya kiganjani, ikiwa picha za watoto, mmoja akionekana kuwa na chini ya umri wa miaka miwili, Grace anasema “nina watoto wawili ambao hawana maambukizi ya Ukimwi, ninaishi vizuri na bado ninaendelea kutumia dawa. » 

Grace katika video ya UNAIDS anajitambulisha jukumu lake akisema, “mimi ni mfamasia wa kijamii, ambapo tunakwenda hospitalini tunachukua dawa na kupatia wagonjwa ambao hawawezi kufika hospitalini kuchukua dawa zao, pengine hawana usafiri, au wanaishi mbali, au kwa sababu ya unyanyapaa hospitalini. Kwa hiyo tunachukua dawa na kuwafikishia nyumbani. » 

Kwa kile afanyacho, Grace anaeleza, “tunapaswa kuwezesha watu hawa watambue kuwa kuishi na virusi vya Ukimwi, hakuondoi ubinadamu wako, la hasha ! bado ni binadamu  na unastahili haki sawa. » 

Na kisha anatamatisha na ujumbe kwa vijana ya kwamba, “unaweza kuwa mtu yeyote unayetaka kuwa bila kujali hali uliyo nayo. » 

Wanawake wajawazito Nigeria hawapati huduma maeneo yanayostahili 

Ripoti iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kuhusu maambukizi ya virusi vya Ukimwi, nchi za Afrika Magharibi na Kati zinashuhudia ongezeko la maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na hivyo kuweka hatarini maisha ya watoto ambao hawajazaliwa.  

DKT.  Akudo Takpeazu Mkurugenzi na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa kudhibiti  Ukimwi na magonjwa ya zinaa nchini Nigeria, (NASCP) anafunguka kile wanachofanya akisema,  “kipaumbele chetu cha kwanza ni kubainisha maambukizi hayo yanatoka wapi ambayo ni mama kwenda kwa mtoto. Kwa hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita tumefanya kazi kubwa. Kwanza kujaribu kutambua na kuelewa ni wapi wanawake hao wote wanakwenda kwa ajili ya kujifungua watoto wao, na iwapo wanapata huduma kabla ya kujifungua.” 

Amesema walichobaini ni kwamba “idadi kubwa ya wanawake hawapati huduma kwenye vituo vinavyotakiwa. Kwa hiyo basi taarifa hizo zimeunda mkakati wetu mpya, na mkakati wetu mpya ni kwenda kusaka wanawake kokote kule waliko.” 

Katika Siku ya Ukimwi Duniani, watu nchini Nigeria walitembea katika kitongoji cha Asokoro huko Abuja ili kuongeza uelewa wa VVU na UKIMWI kwa umma kwa ujumla (faili).
UNAIDS
Katika Siku ya Ukimwi Duniani, watu nchini Nigeria walitembea katika kitongoji cha Asokoro huko Abuja ili kuongeza uelewa wa VVU na UKIMWI kwa umma kwa ujumla (faili).

Kuna ukosefu wa usawa wa huduma miongoni mwa wajawazito 

Akichambua kile kinachochochea changamoto ya Virusi vya Ukimwi zaidi kukumba wanawake nchini Nigeria, Mkurugenzi Mkazi wa UNAIDS nchini humo Leopold Zekeng anasema,“kile kinachoendelea nchini Nigeria ni dhihirisho la ukosefu wa sawa kwa minajili ya huduma za kupunguza  maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto au PMTCT kati ya wanawake ambao wanapata huduma hiyo na wale ambao hawana huduma hiyo ya PMTCT.” 

UNAIDS katika ripoti yake mpya inasema kuwa ubaguzi, unyanyapaa na uharamishaji wa mapenzi ya jinsia moja vinagharimu maisha na kuzuia ulimwengu kufikia malengo yaliyokubaliwa ya ukimwi.  

Nimeusigina unyanyapaa sasa nataka na wengine wafanya hivyo 

Stella Ebeh, Afisa Afya ya Umma huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria anaishi na virusi vya Ukimwi na hakukubali unyanyapaa ukwamishe harakati za kunusuru wengine wanaoishi na virusi hivyo. Akiwa kituo cha afya akitoa huduma kwa wagonjwa anasema“kama mwanamke ninayeishi na virusi vya Ukimwi, nafahamu machungu ya kuishi na virusi hivi. Nafahamu changamoto na sitaki watu wapiti kile nilichopitia kwenye eneo la unyanyapaa. Zamani familia yangu ilininyanyapaa, lakini sasa nimeweza kukabili unyanyapaa na ninausigina kwa miguu yangu.” 

Bi. Ebeh ambaye pia ni mwanchama wa ICW na Mnasihi kwa akina mama wanaoishi na VVU anatamatisha akisema,“hata zaidi ya wagonjwa 7,000 ninaohudumia kwenye kituo cha Mararaba, nimewajengea uwezo wa kukabili unyanyapaa. Nimetumia hali yangu ninayoishi nao kuweka tabasamu kwenye nyuso za watu wanaoishi na VVU. Na nimejiweka mwenyewe kwa sababu nafahamu avaae kiatu ndie afahamuye kinavyombana.”  

Mashirika ya wanawake yapatiwe ufadhili kuondoa pengo la huduma 

Sasa wanawake wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wanajitoa kimasomaso kunusuru wengine lakini changamoto ni rasilimali na ndipo Mkurugenzi wa chama cha kimataifa cha wanawake wanaoishi na virusi vya Ukimwi kanda ya Afrika Magharibi Assumpta Reginald anafunguka ya kwamba “kama wanawake tunaoishi na virusi vya Ukimwi, tunataka kuona rasilimali nyingi zaidi zikielekezwa kwenye mashirika ya wanawake, wanawake wanaoishi na virusi vya Ukimwi. Hii ni kwa sababu kuna kazi nyingi ya kufanya hata kupitia ukatili wa kijinsia na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, lakini mashirika ya wanawake hawana fedha za kutosha.”