Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ili kuumaliza UKIMWI lazima tuweke usawa duniani kote – Katibu Mkuu UN

Mwanamke aliyezaliwa na VVU akipokea dawa kwenye kliniki nchini Burkina Faso
© UNICEF/Frank Dejongh
Mwanamke aliyezaliwa na VVU akipokea dawa kwenye kliniki nchini Burkina Faso

Ili kuumaliza UKIMWI lazima tuweke usawa duniani kote – Katibu Mkuu UN

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa Siku ya UKIMWI Duniani, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe Mosi Desemba, amesema ili kuumaliza ugonjwa huo lazima kwanza kukomesha ukosefu wa usawa ambao unakwaza hatua za kusonga mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu unaohatarisha maisha ya watu ulimwenguni kote.

Bwana Guterres amekumbushia kuwa ulimwengu umeahidi kuumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 lakini wanadamu tuko nje ya njia ya kuelekea kulitimiza lengo hilo. Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu Guterres ametoa wito akisema, “ili kuumaliza UKIMWI, lazima tukomeshe ukosefu wa usawa unaozuia kusonga mbele. Leo, tunahatarisha mamilioni zaidi ya maambukizi mapya na mamilioni ya vifo zaidi. Kwa hiyo, katika Siku hii ya UKIMWI Duniani, tunatoa wito kwa sauti moja. Weka usawa!” 

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa akifafanua kuhusu Kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya UKIMWI Duniani inayosema, "Weka usawa" ni wito wa kuchukua hatua

“Wito wa kupitisha vitendo vilivyothibitishwa ambavyo vitasaidia kumaliza UKIMWI. Upatikanaji zaidi wa huduma za matibabu zilizo bora na zinazofaa, upimaji na kinga ya VVU. Hiyo inamaanisha rasilimali zaidi za kifedha. Sheria bora, sera na desturi za kukabiliana na unyanyapaa na kutengwa wakokabiliana nako watu wanaoishi na VVU, hasa watu waliotengwa. Kila mtu anahitaji heshima na kukaribishwa.” Amefafanua zaidi akieleza hatua hizo zinazotakiwa kuchukuliwa ili kuutokomeza ugonjwa wa UKIMWI. 

Akieleza zaidi kuhusu hatua za kuchukuliwa, Antonio Guterres amesema pia kuwe na ushirikiano bora wa teknolojia ili kuwezesha upatikanaji sawa wa sayansi bora ya VVU, hasa kati ya eneo la Kusini na Kaskazini duniani kote. 

“Kukosekana kwa usawa kunakoendeleza janga la UKIMWI kunawezekana kukomeshwa na lazima kukomeshwe. Tunaweza kumaliza UKIMWI. Ikiwa tutaweka usawa.” Anasisitiza Guterres.  

Takwimu kutoka UNAIDS kuhusu mapambano dhidi ya VVU duniani zinaonesha kwamba katika miaka miwili iliyopita ya COVID-19 na majanga mengine ya kimataifa, maendeleo dhidi ya janga la VVU yamedorora, rasilimali zimepungua, na mamilioni ya maisha yako hatarini. 

“Miongo minne ya mwitikio wa VVU, ukosefu wa usawa bado unaendelea kwa huduma za msingi kama vile kupima, matibabu, na kondomu, na hata zaidi kwa teknolojia mpya.” Inaeleza UNAIDS. 

Aidha takwimu za UNAIDS zinaeleza kuwa wanawake vijana barani Afrika wanasalia kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na VVU, wakati utolewaji wa programu maalum kwa ajili yao unabaki kuwa mdogo sana. Katika nchi 19 zenye mzigo mkubwa barani Afrika, mipango mahususi ya kukinga wasichana balehe na wanawake vijana inafanya kazi katika asilimia 40 pekee ya maeneo yenye maambukizi mengi ya VVU. 

“Ili kuumaliza UKIMWI, lazima tukomeshe ukosefu wa usawa unaozuia kusonga mbele." - António Guterres