Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufukara duniani utaendelea tusipotekeleza mambo matatu- Guterres

Familia maskini na isiyo na makazi huko Yangon nchini Myanmar. Nchi hii  ina mifumo michache ya hifadhi kwa kijamii ambayo inaweza kuitumia
ILO Photo/Marcel Crozet
Familia maskini na isiyo na makazi huko Yangon nchini Myanmar. Nchi hii ina mifumo michache ya hifadhi kwa kijamii ambayo inaweza kuitumia

Ufukara duniani utaendelea tusipotekeleza mambo matatu- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza umaskini duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaja mambo matatu yanayopaswa kufanyika ili harakati zozote za kutokomeza umaskini ambao ametaja kuwa ni kosa la kimaadili kwa zama za sasa uweze kutokomezwa.

 

Guterres ametaja mambo hayo kupitia ujumbe wake wa siku ya kutokomeza umaskini dunia, akisema ni hatua ambazo zinapaswa kuleta marekebisho, ujumuishi na uendelevu.
Amesema mambo hayo matatu ni muhimu ili jamii zilizotumbukizwa zaidi kwenye umaskini kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 ziweze kujinasua kwa usalama na kuwa imara zaidi hata baada ya Corona.

COVID-19 imekuwa mwiba katika maisha ya wengi akisema “kwa mara ya kwanza katika miongo miwili, ufukara unaongezeka. Mwaka jana takribani watu milioni 120 walitumbukia kwenye umaskini baada ya COVID-19 kupomorosha uchumi na jamii. Fursa ya kujikwamua nayo inazidisha ukosefu wa usawa kati ya nchi tajiri na maskini. Mshikamano ambao ndio tuna uhitaji zaidi hivi sasa, haupo.”

Mathalani, ukosefu wa usawa kwenye mgao wa chanjo dhidi ya Corona unaruhusu kuchipuka kwa minyumbuliko mipya ya virusi na hivyo kusababisha vifo zaidi na kuongeza udumavu wa uchumi unaogharimu matrilioni yad ola.

“Lazima tumalize hili janga, tushughulikie suala la madeni na kuhakikisha uwekezaji wa kujikwamua katika nchi ambazo zinahitaij zaidi.” Amesema Guterres.

Akifafanua mambo matatu ya kujikwamua amesema mosi, marekebisho ni muhimu kwa kuwa “hatuwezi kurejea katika mifumo iliyoota mizizi inayoengua wengine na kusababisha ukosefu wa usawa uliokuweko hata kabla ya janga la Corona. Tunahitaji utashi thabiti wa kisiasa kufanikisha hifadhi ya jamii kwa kila mtu ifikapo mwaka 2030 na kuwekeza katika ajira zinazojenga stadi za kazi kwa sekta zisizoharibu mazingira. Tuwekeze pia katika sekta ya malezi ya jamii ili nayo wahusika wapate kipato.”

Jambo la pili ni ujumuishi akisema kujikwamua bila usawa ni kuacha nyuma binadamu wengi ambao tayari walikuwa wameenguliwa na hivyo kutofanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
Mathalani wanawake ambao waliokuwa maskini hata kabla ya Corona idadi yao ilikuwa ni ya juu akisema, “wanaume 22 matajiri zaidi duniani, utajiri wao ni zaidi kuliko ule wa wanawake wote barani Afrika.”

Kipengele cha tatu ni uendelevu akisema ni muhimu “kwa sababu tunahitaji kujenga mnepo, tuondoe hewa chafuzi na tusizalishe kabisa hewa za ukaa.”
Ametaka jamii kutumia siku ya leo na kila siku kushikamana kutokomeza umaskni na kujenga dunia yenye haki, utu na fursa kwa wote.