Radio inakwenda na wakati kukidhi mahitaji ya jamii- UNESCO

13 Februari 2021

Leo ni siku ya redio duniani, siku ambayo huadhimishwa kila tarehe 13 ya mwezi Februari kutoa fursa ya kuangazia mabadiliko, ubunifu na uunganishaji wa chombo hicho ambacho kimetimiza miaka 110.
 

Maudhui ya mwaka huu ni Dunia Mpya Redio Mpya ikilenga kuonesha mnepo wa redio na uwezo wake wa kubadilika au kwenda sambamba na mabadiliko ya kwenye jamii na mahitaji ya wasikilizaji.

Katika kuadhimisha siku hii, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Audrey Azoulay, ameitaja redio kuwa ni wakala wa uhuru na kwamba chombo hicho kitaendelea kuwa muhimu katika jamii za sasa.

Chombo kinachobadilika

Kadri dunia inavyobadilika, vivyo hivyo kwa redio ambayo inaendelea kunakili historia ya binadamu na kuendana na mazingira yake.

Hali hiyo imekuwa muhimu sana na dhahiri wakati wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, ambapo redio imewezesha kuendelea kwa mafunzo na kukabiliana na kusambaa kwa taarifa potofu.

“Janga la COVID-19 limetukumbusha thamani ya ziada ya redio: ikiwa inafikia zaidi ya asilimia 75 ya wakazi katika nchi zinazoendelea, radio inasalia kuwa chombo kinachofikia watu wengi zaidi,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNESCO akisema ndio maana redio imekuwa mbinu ya msingi wakati wa hatua dhidi ya janga la Corona.

Mtoto akisoma kwa njia ya redio
UNICEF/Habib Kanobana
Mtoto akisoma kwa njia ya redio

Amesema radio imeokoa maisha kwa kuwezesha kusambaza taarifa za uhakika za afya na kukabiliana pia na taarifa za chuki.

UNESCO iliandaa ujumbe huru katika lugha 56 na kuzisambaza kwa vituo vya redio kote ulimwenguni ili kukabiliana na taaarifa potofu.

Redio na teknolojia mpya

Ili kuweza kufikia mtu popote pale alipo na kila mtu wakati huu wa maendeleo ya teknolojia, redio nayo imebadilika.

Wakati redio za zama za kali ilikuwa ni transista rahisi inayowekwa kwenye meza jikoni au verandani na kusikilizwa na wengi, hivi sasa redio inapatikana kwenye simu janja na kukufuata popote pale msikilizaji anapokwenda.

Hivi sasa redio siyo tu chombo cha kupata sauti, bali pia kutokana na maendeleo ya teknolojia imeweza kwenda na mitindo na tabia za wasikilizaji.

Hi leo redio inasikilizwa kupitia televisheni wakati vipindi aina ya podiskasti vinaweza kupakuliwa na msikilizaji na kusikilizwa wakati wowote ule apendao.

Ni kwa mantiki hiyo Bi. Azoulay anasema kuwa redio inasalia kuwa chombo muhimu ambacho kinathibitisha mnepo wa kila siku sambamba na uwezo wake wa kwenda na wakati.

Akitambua kuwa hii ni karne ya taswira, Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNESCO amesema redio inajenga taswira na fikra za dunia ambazo lazima zisikilizwe ndipo zieleweke. “Kutokana na uwepo wa matangazo ya redio kupitia intaneti, vipindi vya podikasti, simu janja na teknolojia mpya, nidhahiri kuwa redio ‘imebalehe’ tena na kurejea tena ujanani.”

Redio ni kiunganishi

Redio pia inahudumia jamii na kusambaza taarifa muhimu wakati wa majanga asili, majanga ya kiuchumi na kijamii, milipuko ya magonjwa na hata matukio mengine muhimu.

Matangazo ya umma, maonyo na matangazo mengine ni sehemu tu ya jinsi redio inatumika kukidhi mahitaji muhimu ya wasikilizaji wake.

Bi. Azoulay amesema redio inaunganisha wat una kujenga uhusiano na kwamba kuliko wakati wowote ule, tunahitaji chombo hiki cha kiutu duniani.

Amesisitiza kuwa bila redio, haki ya uhuru wa kupata habari na kujieleza na aina zingine zote za uhuru wa msingi ingalidhoofishwa sambamba na uhuru wa utofauti kwa kuwa redio hususan redio za kijamii ni vituo vya kupaza sauti za wasio na maeneo ya kupazia sauti.

Ni kwa mantiki hiyo katika siku ya redio duniani, Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNESCO ametoa wito kwa kila mtu, wasikilizaji, watangazaji na wataalamu wa sauti na picha kusherehehea siku hii na maadili yake na kuendeleza taarifa za uhakika kwa maslahi ya kila mtu.

Apu ya Habari za UN
Umoja wa Mataifa
Apu ya Habari za UN

Radio ya Umoja wa Mataifa

Siku ya redio duniani tarehe 13 Februari ni siku ambayo redio ya Umoja wa Mataifa ilianzishwa. Redio hiyo ilianza rasmi matangazo yake tarehe 13 mwezi Februari mwaka 1946 kutokea katika studio za muda na ofisi za Umoja wa Mataifa huko Lake Success jiijni New York ambapo matangazo ya kwanza kabisa yalisema, “Huu ni Umoja wa Mataifa ukiita watu wa dunia.”

Redio ya Umoja wa Mataifa ilianzishwa na azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa namba 13 (1) ikiipatia Idara ya Taarifa kwa Umma ya chombo hicho mamlaka ya kuanzisha Radio ya Umoja wa Mataifa kwa kutambua kuwa Umoja wa Mataifa hauwezi kufanikisha malengo yake ya kuanzisha iwapo wananchi wa dunia hawahabarishwi ipasavyo kuhusu malengo na shughuli zake.

Katika utafiti uliofanywa na Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa mwezi Novemba na Desemba mwaka 2016, vituo vidogo vya redio ambavyo Idhaa za Umoja wa Mataifa ni washirika wao, zilisema kuwa taarifa za kimataifa kutoka idhaa hizo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa redio nyingi ndogo hazina uwezo wa kupata au kuandaa taarifa hizo wao wenyewe.

Redio ya UN nayo yaenda na wakati

Mwaka 2017, Redio ya Umoja wa Mataifa iliungana na kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa na kuunda UN News ambapo idhaa zinaandaa taarifa za habari kwa sauti na maandishi, picha na video kwa lugha 9 ambazo ni Kiswahili, Kiarabu, Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kispayola, Kireno, Kirusi, na Kihindi kwa ajili ya wasikilizaji kupitia wavuti zao na radio,televisheni na blogu washirika zaidi ya 2,000 duniani kote.

Hivi sasa matangazo ya UNNews yanapatikana kwenye intaneti, apu za radio kama Tune In, kwenye simu janja kupitia apu ya UN News.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter