Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa kuhifadhi mikoko Senegal waongeza pia kipato cha wavuvi wa chaza

Mikoko inasadia kutunz mazingira ambayo husaidia mazao ya baharini kuwa na faida
Manglar Vivo Project, UNDP Cuba
Mikoko inasadia kutunz mazingira ambayo husaidia mazao ya baharini kuwa na faida

Mradi wa kuhifadhi mikoko Senegal waongeza pia kipato cha wavuvi wa chaza

Tabianchi na mazingira

Nchini Senegal, mradi wa pamoja wa mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo duniani, IFAD na serikali ya taifa hilo la Afrika Magharibi umesaidia kurejeshwa upya kwa maelfu ya hekta za mikoko baharini na hivyo kusaidia jamii za wavuvi kuinua kipato chao na wakati huo huo kuwa na  mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Nyakati za asubuhi Mariane na wanawake wenzake wakiwa kwenye boti kwa kwa furaha na matumaini ya kuvua kiasi cha kutosha cha Kamba na chaza kwenye bonde la Saloum lililoko eneo la Fatick nchini Senegal. Miaka 10 iliyopita eneo hili lilikuwa kame baada ya takribani asilimia 40 ya mikoko kutoweka sambamba na eneo la mazalia ya chaza na Kamba kuanzia miaka ya 1970. 

Mradi wa kurejesha mikoko unaondeshwa na serikali ya Senegal na IFAD umesaidia pia kuepusha eneo la ardhi kumegwa na bahari na hivyo kuleta nuru kama asemavyo Marianne. “Kurejeshwa kwa mikoko ni muhimu sana. Hii leo bahari haijameza kijiji chetu. Tunashukuru mradi kwa kuwa kama hatua isingalichukuliwa, kijiji chetu kingetoweka. Unapohifadhi misitu unaona tope kwenye mikoko, na tope linazuia mawimbi ya bahari na hivyo bahari haiwezi tena kumeza kijiji chetu.” 

Mikoko ni muhimu katika kuzuia mmomonyoko wa udongo na pia ni mazalia ya viumbe vya baharini. Hata hivyo miaka 25 iliyopita, Afrika imepoteza takribani hekta 500,000 za mikoko kutokana na ukame, ukataji miti hovyo na ujenzi. 

Yotsna Puri ambaye ni Mkurugenzi wa Mazingira, Tabianchi, Jinsia, Vijana na Lishe IFAD anapatia msisitizo hoja ya uhifadhi wa mikoko. “Ni muhimu sana kuhifadhi maeneo ya misitu ya mikoko inayozingira Senegal kwa sababu inakuwa ndio kingo la mwisho la mnepo kwa nchi kama hii. Ukataji kiholela wa mikoko, ujenzi vimesababisha mmomonyoko wa maeneo kama haya hivyo ikimaanisha kwamba njia za jamii kujipatia kipato zinatoweka  na hilo ndio jambo ambalo IFAD inajaribu kurekebisha hivi sasa.”

Mradi huu umenufaisha zaidi ya kaya Elfu 50 kwenye eneo la Fatick nchini Senegal kwa kuwapatia mikopo na mafunzo ya jinsi ya kuongeza thamani kwenye mazao yao ikiwemo chaza. 

Marianne na wenzake wamenufaika na sasa wanakausha chaza na kuwasindika kwenye chupa. “Nilipoanza hii biashara, sikufahamu mambo mengi. Sikufahamu kuwa naweza vuna chaza au hata kuwaweka kwenye kitalu wazaliane. Sasa hivi nachukua chaza, nawachemsha na kuwakausha. Kwa kuwasindika tunapata fedha zaidi. Karai moja la chaza hupati fedha nyingi kama vile ukisindika na kuwaweka kwenye chupa.” 

Kwa kupata kipato cha ziada, inamaanisha Mariane anawea kulipa karo za shule za watoto wake na kuwanunua mavazi. 
Lengo la IFAD ni kurejesha zaidi ya hekta nyingine 1,000 katika miaka michache ijayo.