Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na UNICEF zataka kuanzishwa kwa safari za ndege maalum kupeleka misaada Afghanistan

Zaidi ya familia 400 zinaishi kwenye makazi ya muda katika shule Kaskazini mwa Kabul, mji mkuu wa Afghanistan
© UNICEF Afghanistan
Zaidi ya familia 400 zinaishi kwenye makazi ya muda katika shule Kaskazini mwa Kabul, mji mkuu wa Afghanistan

WHO na UNICEF zataka kuanzishwa kwa safari za ndege maalum kupeleka misaada Afghanistan

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametaka kuanzishwa mara moja kwa daraja maalum la safari za ndege la kuwezesha ndege zilizobeba misaada ya kibinadamu kuingia nchini Afghanistan kwa ajili ya utoaji wa msaada endelevu na bila vizuizi. 

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa ni lile la Afya Ulimwenguni WHO na la Kuhudumia watoto UNICEF ambayo yametoa wito huo wakati Uwanja wa ndege wa Kabul ukiwa umefungwa baada ya Taliban kushika madaraka ya nchi hiyo ilihali kuna uhitaji wa kusambazwa dawa na vifaa vingine vya matibabu ya mamilioni ya watu ikiwemo zaidi ya watu 300,000 ambao wameyakimbia makazi yao katika kipindi cha miezi miwili iliyopita pekee.

Taarifa ya pamoja ya mashirikia hayo mawili imeeleza kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu huku uwezo wa kusambaza misaada hiyo ukizidi kupungua. 

Mkurugenzi wa WHO kwa ukanda wa Mashariki na Mediterania Dkt Ahmed Al Mandhari  katika taarifa hiyo amesema, “Kwasiku kadhaa macho yote yameelekea kutazama hali iliyopo katika uwanja wa ndege wa Kabul ambapo zoezi la kuwaondoa wafanyakazi wa kimataifa na wa Afghan walio katika hatari, lakini msaada wa kibinadamu unaowakabili wananchi wengi hautakiwi -na hauwezi kupuuzwa. Hata kabla ya tukio lililotokea wiki chache zilizopita m Afhanistan ilikuwa nchi ya tatu duniani yenye kuendesha usaidizi mkubwa wa kibinadamu, ikiwa na watu zaidi ya milioni 18 wenye kuhitaji msaada.” 

 WHO na UNICEF tumedhamiria kuendelea kubaki na kusaidia wananchi wa Afghanistan.

Kwa hali iliyopo sasa ya ndege za kawaida kuzuiwa kutua katika uwanja wa ndege wa Kabul, hatuna njia ya kuwezesha misaada kuingia nchini humo na kuwafikia wahitaji. Si kwa mashiriika ya Umoja wa Mataifa pekee bali hata mashirika mengine ya misaada pia wanakabiliwa na tatizo hilo hilo.

Mkurugenzi wa UNCEF kanda ya Asia kusini George Laryea-Adjei amesema "Katika siku za mwanzo baada yaTaliban kuchukua uongozi wa Afghanistan, WHO na UNICEF - kama mashirika mengine yote ya UN - zilitanguliza ulinzi na usalama wa wafanyikazi wetu. Lakini kazi yetu iliendelea hata wakati hali ilikuwa mbaya zaidi. Tunabaki kujitolea kukaa Afghanistan na kutoa huduma, na tulihamisha mfumo wa utendaji wetu haraka kushughulikia mahitaji ya mamilioni ya Waafghan ambao wanabaki nchini.”

Machafuko yanayoendelea nchini humo, watu wengi kuyakimbia makazi yao, ukame na janga la COVID-19 vyote vinachangia hali ngumu na ya kutatanisha nchini Afghanistan. Mashirika ya kibinadamu yamekuwa yakieleza kila uchwao kuhitaji kuungwa mkono na kuwezeshwa ili kukidhi mahitaji makubwa na yanayoongezeka nchini Afghanistan, na kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayekufa kwa sababu ya ukosefu wa msaada.