UNICEF yatangaza kupanua huduma kwa wanawake na waoto nchini Afghanistan

23 Agosti 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema linaongeza programu zake za kuokoa maisha ya watoto na wanawake nchini Afghanistan ikiwa ni pamoja na kupitia huduma za afya, lishe na maji kwa familia zilizoyakimbia makazi yao. 

Taarifa iliyotolewa leo mjini New York nchini Marekani na Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore juu ya watoto nchini Afghanistan imesema wanatarajia kupanua shughuli hizo kwa maeneo ambayo hapo awali hayangeweza kufikiwa kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

Fore amesema mpak hii leo, karibu watoto milioni 10 nchini Afghanistan wanahitaji msaada wa kibinadamu ili waweze kuishi. 
Watoto milioni 1 wanakadiriwa kuugua utapiamlo mkali katika kipindi cha mwaka huu  wa 2021 na wanaweza kufa bila matibabu. 
"Huu ni ukweli mbaya unaowakabili watoto wa Afghanistan na unabaki hivyo bila kujali maendeleo ya kisiasa na mabadiliko katika serikali. Tunatarajia kuwa mahitaji ya kibinadamu ya watoto na wanawake yataongezeka kwa miezi ijayo katikati ya ukame mkali na uhaba wa maji, matokeo mabaya ya uchumi na uchumi wa janga la COVID-19 na mwanzo wa msimu wa baridi.”amesema Fore

Fore ametuma ujumbe maalum kwa uongozi nchini Afghanistan wakati wafanyakazi wa UNICEF wakitekeleza majukumu yao
"Tunawahimiza Taliban na makundi mengine kuhakikisha UNICEF na washirika wetu wa masuala ya kibinadamu wanaweza kuwafikia watoto kwa usalama na bila ya vipingamizi mahali popote ambapo tunaenda kutoa msaada kwa wenye uhitaji. Nasisitiza, wahusika wote wa masuala ya kibinadamu lazima wawe na nafasi ya kufanya kazi kulingana na kanuni za haki za kibinadamau, utu, kuvumiliana , kutopendelea na kwa uhuru.”

Tangu mwezi Januari 2021, Umoja wa Mataifa umerekodi ukiukaji mkubwa wa haki za watoto. Takriban watoto na wanawake 435,000 wameyakimbia makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani.

 
 
 
 
 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter