Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wekeni silaha chini wakati wa mashindano ya Olimpiki: Guterres

Mashindano ya Olimpiki yamepangwa kuanza tarehe 23 Julai 2021, baada ya kucheleweshwa mwaka mmoja kutokana na janga la Corona
Unsplash/Erik Zünder
Mashindano ya Olimpiki yamepangwa kuanza tarehe 23 Julai 2021, baada ya kucheleweshwa mwaka mmoja kutokana na janga la Corona

Wekeni silaha chini wakati wa mashindano ya Olimpiki: Guterres

Amani na Usalama

Kuelekea ufunguzi wa mashindano ya Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan tarehe 23 mwezi huu wa  Julai, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka utamaduni wa kusitisha mapigano wakati wa mashindano hayo uheshimiwe duniani kote. 

Katika ujumbe wake kwa njia ya video Guterres amesema, “washiriki wa mashindano haya ya kawaida na yale ya watu wenye ulemavu wamevuka vikwazo vingi mpaka kufikia kushiriki mashindano hayo, katika kipindi chote cha janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.”

Amesema kutafuta amani na mshikamano katika malengo yanayofanana ni muhimu zaidi mwaka huu wakati dunia inapambana kumaliza janga la Corona na kujenga upya ulimwengu ulio imara na endelevu.

Guterres ameongeza kuwa “wananchi wanaoishi katika maeneo yenye machafuko watapumzika kusikia milio ya risasi na pengine itakuwa mwanzo mzuri wa kukaa na kujadiliana pamoja katika kutafuta amani ya kudumu”. 

Usitishaji wa mapigano au kuweka silaha chini wakati wa mashindano ya michezo ya Olimpiki ni utamaduni wa miaka mingi uliolenga kuwahakikishia usalama wachezaji na watu wote wanaojumuika katika mashindano hayo makubwa duniani.