Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Radio ngangari licha ya maendeleo ya teknolojia – Guterres

Radio inaendelea kushamiri hata kwenye viwanja vya michezo
UNESCO
Radio inaendelea kushamiri hata kwenye viwanja vya michezo

Radio ngangari licha ya maendeleo ya teknolojia – Guterres

Utamaduni na Elimu

Leo ni siku ya radio duniani, ikitambua kuanzishwa kwa Radio ya Umoja wa Mataifa mwaka 1946. Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO liliridhia kuadhimishwa kwa siku hii wakati wa kikao cha bodi yake tendaji  cha tarehe 29 mwezi Septemba mwaka 2011.

Ikiwa leo ni siku ya radio duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa Antonio Guterres amesema licha ya maendeleo ya teknolojia, bado radio imesalia chombo adhimu katika kuleta jamii pamoja na kuwezesha watu kufikia uwezo wao wa juu zaidi kimaisha.

Katika ujumbe wake wa siku ya leo yenye maudhui redio na michezo, Bwana Guterres amesema

 (Sauti ya Antonio Guterres)

“Katika zama za maendeleo makubwa zaidi ya mawasiliano, radio imebaki na uthabiti wake wa kuelimisha, kuburudisha, kuhabarisha na kuhamasisha. Inaweza kuunganisha na kujengea uwezo jamii na kuwapatia sauti watu wa  wa pembezoni.”

Na katika michezo ameenda mbali na kutoa mfano akisema..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Mwaka huu mashindano ya olimpiki ya majira ya baridi yakiendelea, tunatambua njia mbalimbali ambazo kwao utangazaji wa michezo unaleta watu pamoja katika msisimko na mafanikio.”