Tochi ya Olimpiki iangazie mshikamano wa amani kimataifa:Guterres
Juma hili maelfu ya watu na hususani wanamichezo wanakusanyika mjini PyeongChang huko Jamhuri ya Korea, kwa ni ya kushiriki mashindano ya Olimpiki ambayo ni ya kirafiki, yenye mshikamano, na ya kuheshimiana.
Katika ujumbe wake maalumu kwa ajili ya michezo hiyo ya Olimpiki inayojumuisha pia Olimpiki ya walemavu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hushirikisha wanariadha bora duniani na kwamba mashindayo hayo yaliyoanza katika enzi za Ugiriki ya kale, yanatoa nafasi kwa washiriki wanariadha na watazamaji, kusafiri kwa amani na pia kudumisha amani miongoni mwa washiriki wakati wote michezo inapofanyika.
Na kwa mantiki hiyo amesema “jamii yetu inaweza kuvuka tofauti zote za kisiasa”. Akiongeza kuwa inaenda sanjari na wakati wa sasa hasa katika rasi ya Korea, akitoa wito kwa pande zote husika katika mgogoro wa rasi hiyo kuheshimu dhamira ya olimpiki wakati wa michezo ya 2018 ya olimpiki ya kawaida na ile ya walemavu.
Amechagiza na hebu mwanga wa Olimpiki umulike kama ishara ya mshikamano wa binadamu wote, na dhamira ya Olimpiki isaidie kusambaza utamaduni wa amani.
Naye mwanariadha nyota mkimbizi wa Sudan kusini, Yiech Pur Biel ambaye tayari yuko PyeongChang kwa ajili ya mashindano hayo amebeba ujumbe maalumu kwamba “Amani ni msingi wa kila kitu ambacho serikali inaweza kufanya, na kila hatua kuelekea amani ni muhimu”.
Pur Biel alilazimika kukimbia machafuko Sudan Kusini mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 10 tu akiwaacha nyuma wazazi wake na kwenda kuishi kambi ya Kakuma nchini Kenya.
Amesema amehamasishwa kwamba wawakilishi wa Korea ya Kaskazini (DPRK) na Jamhuri ya Korea Kusini watatembea pamoja wakipeperusha bendera ya Olimpiki katika mashindano hayo yatakayoanza rasmi kesho Februari 9.