Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu imegeuzwa mtaji hivi sasa duniani- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwasilisha ripoti yake ya mwaka kuhusu kazi za Umoja wa Mataifa
UN Photo/Cia Pak
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwasilisha ripoti yake ya mwaka kuhusu kazi za Umoja wa Mataifa

Hofu imegeuzwa mtaji hivi sasa duniani- Guterres

Masuala ya UM

Mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74 umeanza leo kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema kuwa hofu imetanda duniani hivi sasa na ni jukumu la viongozi kuondoa hofu hiyo miongoni mwa wananchi wao.

Akiwasilisha mbele ya viongozi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa ripoti yake ya mwaka kuhusu utendaji wa Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu Guterres amesema katika safari zake ameshuhudia madhila kuanzia Pasifiki kusini watu wanahofia maisha yao kusombwa na mawimbi ya baharí hadi manusura wa Ebola huko nchini DR Congo wanaohaha kujenga upya maisha yao.

Guterres amesema, “tunaishi kwenye ulimwengu uliosheheni hofu. Watu wengi wana hofu ya kukandam izwa, kuchukizwa au kuenguliwa na kuachwa nyuma. Mashine zinachukua ajira zao, wasafirishaji haramu wanateka  utu wao, wababe wa kivita wanachukua uhai wao, nishati ya kisukuku inapora mustakabali wao.”

Hata hivyo amesema kwa kuwa bado watu wana imani na misingi ya Umoja wa Mataifa  “lakini je wanatuamini sisi ? je wanaamini kuwa viongozi wanaweka mbele maslahi ya watu. Sisi viongozi tunapaswa kuhudumia wananchi.”

MVUTANO BAINA YA MATAIFA

Katibu Mkuu akamulika pia kipindi cha sasa cha mpito na ukosefu wa uhusiano bora wa kimataifa akisema, “mvutano huo unaweza kuwa si mkubwa lakini ni kitu halisia.

“Nahofia mpasuko mkubwa: dunia inagawanyika katika vipande viwili, ambapo mataifa mawili yenye uchumi mkubwa duniani yanaunda pande mbili tofauti za ushindani, kila upande ukiwa na sarafu yake thabiti, mtandao wake wa intaneti na uwezo wa akili bandia, AI na mikakati yao ya kijeshi,” amesema Guterres.

Kwa mantiki hiyo amesema, “ ni lazima tufanye kila tuwezalo kuepusha mpasuko huo mkubwa na tuendeleze mfumo wa umoja, uchumi wa pamoja unaoheshimu sheria za kimataifa, dunia thabiti ya kimataifa yenye taasisi thabiti za kimataifa,” amesema Guterres.

Tweet URL

HOFU IMETANDA NA NDIO BIDHAA IUZAYO ZAIDI DUNIANI

Katibu Mkuu akageukia suala la ukosefu wa imani hivi sasa duniani akisema kuwa kutengwa na kukosa imani vimekuwa ni silaha, “hofu ikiwa bidhaa inayouza zaidi hivi sasa duniani,” akikumbusha kuwa kwa wale wanaosisitiza ukandamizaji au mgawanyiko, “nawaeleza kuwa utofauti ni  utajiri katu si tishio.”

Amesema kuwa haikubaliki kuwa katika karne ya 21 wanawake na wanaume wanateswa kwa sababu ya  utambulisho wao, imani zao au jinsia zao.

TUNASHUHUDIA UKOSEFU WA USAWA WA JINSIA HATA KWENYE MIKUTANO HII

Kuhusu  usawa wa jinsia amekumbusha kuwa katu watu wasisahau kuwa usawa wa jinsia ni suala la  mamlaka, “na madaraka bado yamejikita kwa wanaume kama tunavyoona kuanzia kwenye mabunge hadi vyumba vya mikutano n ahata wiki hii kwenye kumbi, vyumba vya mikutano vya Umoja wa Mataifa.”

Amesema hali hiyo inamaanisha ni kuendelea kurudisha nyumba  haki za wanawake. Kwa mwelekeo wa sasa, itachukua karne mbili kuziba pengo la uwezeshaji wa kiuchumi. Hatuwezi kukubali dunia ambayo inawaeleza wajukuu zangu kuwa usawa unapaswa kusubiri hadi kwa vitukuu wa vitukuu wao.

Kwa mantiki hiyo amesema ni lazima viongozi kwenye ukumbi huo wakidhi matakwa ya wananchi akisema kuwa, “katika zama hizi za mgawanyiko lazima turejelee upya kwenye kusudio. Hebu turejeshe imani, tujenge matumaini na tusonge mbele pamoja.”