Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa waitaka Iran imwachie huru mwanazuoni Xiyue Wang.

Muonekano wa mji wa Tehran nchini Iran Desemba, 11, 1997.
UN Photo/Milton Grant
Muonekano wa mji wa Tehran nchini Iran Desemba, 11, 1997.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa waitaka Iran imwachie huru mwanazuoni Xiyue Wang.

Haki za binadamu

Wataalam wa Umoja wa Mataifa wameisihi Iran imwachie haraka mwanazuoni Xiyue Wang wakidai kushikiliwa kwake kinyume cha utaratibu kwa takribani miaka mitatu ni ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu chini ya sheria za kimataifa.

Taarifa iliyotolewa leo hii na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa,  OHCHR mjini Geneva Uswisi, imeeleza kuwa Wang raia wa Marekani aliyezaliwa China ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa uzamivu katika Chuo Kikuu cha Princeton alikamatwa mnamo mwezi Agosti mwaka 2016 nchini Iran ambako alikuwa anafanya utafiti kwa ajili ya masomo yake kuhusu historia ya eneo la bara Ulaya na Asia yaani Eurasia. 

Mwezi Julai 2017 mahakama ilimpata Wang na kosa la kupeleleza siri za nchi na kushirikiana na watu wengine na hivyo akahukumiwa kifungo miaka 10 jela kupitia hukumu iliyofanyika bila kuruhusu uwazi kwa watu wengine kushuhudia. 

Taarifa ya OHCHR inasema afya ya Wang inaripotiwa kuendelea kuzorota na maisha yake yako hatarini kutokana na madai kuwa aliteswa alipokuwa kizuizini. 

Wajumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa akiwemo wa kuhusu uhuru wa kujieleza, David Kaye,  mjumbe wa Iran Javaid Rehman na yule anayeshughulikia matendo ya kushikiliwa pasipo kufuata utaratibu wamesema “mamlaka za Iran kutumia tuhuma za upelelezi wa siri za nchi dhidi ya Bwana Wang kwa kuwa tu aliomba kibali cha kuona nyaraka za kihistoria ni hali ambayo ni ya kipuuzi. Mazingira ya uendeshaji wa kesi katika mazingira ya faragha kunatuletea wasiwasi kuhusu kesi hii.”