Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yawezekana kumaliza mabomu ya kutegwa ardhini Sudan Kusini:UNMAS

zoezi la uteguzi wa mabomu ya ardhini katika uwanja wa ndege wa Kidal Septemba 2015 kabla ya ziara ya Kamanda wa Jeshi la Ujumbe huo
UN Photo/Marco Dormino
zoezi la uteguzi wa mabomu ya ardhini katika uwanja wa ndege wa Kidal Septemba 2015 kabla ya ziara ya Kamanda wa Jeshi la Ujumbe huo

Yawezekana kumaliza mabomu ya kutegwa ardhini Sudan Kusini:UNMAS

Amani na Usalama

Tatizo la mabomu ya kutegwa ardhini ni kubwa nchini Sudan Kusini kutokana na vita vinavyoendelea, na mabomu hayo ni tishio kwa maisha na usalama wa watu, hata hivyo Umoja wa Mataifa nchini humo unasema inawezekana kuchukua hatua na kumaliza mabomu hayo.

Akizungumzia matumaini kutokana na kazi kubwa wanayoifanya Sudan Kusini katika kutegua na kuondoa mabomu ya ardhini Richard Boulter ambaye ni maneja wa program ya Umoja wa Mataifa ya kutoa huduma ya hatua dhidi ya mabomu ya ardhini UNMAS nchini humo amesema, “Sudan Kusini inawezekana, tuko katika hatua za mwisho sasa na tunahitaji msaada ili kufanikisha hili. Sio tatizo la miaka elfumoja, sio tatizo la miaka mia, ni tatizo la miaka mitatu hadi mitano na kisha litatoweka.”

Boulter ambaye amejitolea maisha yake kwa zaidi ya miaka 25 sasa kukabiliana na vifaa ya milipuko anasema tangu mwaka 2004 ofisi ya Umoja wa Mataifa imekuwa ikisimamia uteguaji wa mabomu, kuyaharibu, na kuyaondolea uwezo wa kulibuka zaidi na mabomu na vifaa vya mlipuko milioni moja Sudan Kusini. Ameongeza kuwa kuna idadi kubwa na namba nyingi zingine ndogo na nyingine kubwa lakini “mwisho wa siku kuna namba mbili tu ambazo ni za muhimu sana , moja ni za mambomu ambayo bado yanahitaji kuteguliwa na kuondolewa na ya pili ni idadi ya watu ambao wanaathirika au kuumia na mabomu na vifaa hivyo vya mlipuko.”

Amesema mwaka jana Sudan Kusini ilifikia idadi mbaya ya watu 5000 waliouawa au kujeruhiwa na vifaa vya mlipuko ikiwemo mabomu ya kutegwa ardhini. Lakini anasema kutokana na juhudi za UNMAS sasa idadi imekwenda chini kwa kiasi kikubwa na pia uelimishakji kuhusu athari za vifaa hivyo kwa jamii imesaidia.

Na katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu mabomu na msaada katika hatua dhidi ya mabomu hayo ambayo kila mwaka huadhimishwa Aprili 4 Boulter anasema kaulimbiu mwaka huu ni “usalama viwanjani- usalama majumbani” akisema ni muhimu shana kwa sababu hivi sasa jumuiya ya kimataifa ikijiandaa na wimbi kubwa la wakimbizi wa ndani kurejea majumbani kwao. Amesisitiza “ni muhimu kuhakikisha kwamba wanakorejea ni salama ili waweze kujenga upya maisha yao.”

Na kwa hilo amesema wana kibarua kigumu na cha muhimu ambacho mosi ni kusafisha mazingira kwa kuondoa vilipuzi vyote  na pili ni  kuchagiza kujiamini na kuwapa watu taarifa ili waweze kuthubutu kutumia tena ardhi zao, kwani tunahitaji kushirikisha jamii , kusikia hofu zao na kuzishughulikia.