Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu habarishi na burudishi imeokoa watoto dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini Ukraine

Jopo la watendaji wakitegua mabomu yaliyotegwa ardhini huko Equatoria ya Kati nchini Sudan Kusini
UNMISS/JC McIlwaine
Jopo la watendaji wakitegua mabomu yaliyotegwa ardhini huko Equatoria ya Kati nchini Sudan Kusini

Elimu habarishi na burudishi imeokoa watoto dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini Ukraine

Amani na Usalama

Hii leo ikiwa ni miaka 20 tangu kuanza kutumika kwa mkataba wa kimataifa dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini na vilipukaji, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetaka hatua zaidi dhidi ya silaha hizo ambazo imesema hazina macho.

Rebecca Morris anajisikia salama baada ya uteguaji wa mabomu uliofanywa na UNMAS
UNMAS
Rebecca Morris anajisikia salama baada ya uteguaji wa mabomu uliofanywa na UNMAS

Ted Chaiban mkuu wa programu kutoka UNICEF amesema hayo wakati wa tukio maalum la maadhimisho hayo mjini New York, Marekani, tukio lililoandaliwa kwa pamoja na shirika hilo na wadau wengine ikiwemo Norway ambayo inashikilia urais wa mkataba huo.

Athari za mabomu kwa watoto

Bwana Chaiban amesema “silaha hiyo isiyo na jicho inapolipuka haichagui kama inashambulia watoto, watu wazima, basi lililobeba watoto wa shule au la na madhara yake ni makubwa na ni ya maisha.”

Ametaka hatua thabiti zichukuliwe kwa kuwa mashambulizi yatokanayo na mabomu ya kutegwa ardhini yanakiuka mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC ambao unataka watoto walindwe.

Wakati wa tukio hilo video mahsusi ya UNICEF kutoka Ukraine ilionyesha jinsi watoto nchini humo wanavyoishi kwa hofu kutokana kwa kuenea kwa mabomu yaliyotegwa ardhini.

Ukraine mfumo wa kawaida wa kuelimisha uligonga mwamba

Akizungumza katika jopo la watoa mada, mtaalamu wa UNICEF kutoka Ukraine Sergiy Prokhorov amesema mabomu hayo ni rahisi kutega lakini magumu kutegua na yameongeza hofu zaidi kwa watoto nchini humo ambao tayari walikuwa wanaogopa wanajeshi.

Amesema uelewa wa watoto kuhusu hatari zitokanazo na mabomu hayo ulikuwa ni mdogo mno na hata walipoamua kutumia njia za kawaida wa kuelimisha watoto kupitia radio hazikuzaa matunda.

“Tulitumia njia tofauti za burudani lakini zinazoelimisha na watoto walifurahi na walishiriki kujifunza kuhusu hatari za mabomu hayo,” amesema Bwana Prokhorov akiongeza kuwa walitumia pia njia ya kufundisha watoto watakaolimisha watoto wao na imezaa matunda.

Bwana Prokhorov amesema hadi sasa kampeni kupitia video, sauti na mabango imefikia watoto zaidi ya milioni 3.1 nchini Ukraine na watoto 600 waelimishaji rika walifuzu.

Suzan Kiden Dominic, mteguaji mabomu aliyefundishwa na UNMAS
UNMAS
Suzan Kiden Dominic, mteguaji mabomu aliyefundishwa na UNMAS

Msumbiji  yajinasibu kutegua mabomu  yote yaliyokuwa yametegwa ardhini

Mapema Mwakilishi wa kudumu wa Msumbiji kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi António Gumende, alizungumzia mafanikio ambayo nchi yake ilipata katika kutegua mabomu  yaliyokuwa yametapaa nchini humo kutokana na vita vya ukombozi na vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya uhuru.

“Msumbiji ilikuwa ni moja ya nchi  yenye idadi kubwa zaidi ya mabomu ya kutegwa ardhini na tulijulishwa kuwa ingalituchukua kati ya miaka 50 hadi 100 kutegua mabomu yote,” amesema Balozi Gumende.

Hata hivyo amesema mwaka 1994 walipoanza kazi ya kutegua mabomu hayo kwa msaada wa Umoja wa Mataifa na wadau wake, waliweza kuondoa mabomu yote ilipofika mwaka 2016 akitaja sababu ya mafanikio kuwa ni utashi wa kisiasa wa serikali, ushirikishaji wananchi pamoja na wadau wa nje.

Amesema ingawa mabomu ya kutegwa ardhini hakuna tena, athari zilizopata manusura bado zipo na hivyo wataendelea kushikamana na mkataba huo ili kuwatendea haki manusura hao.

Mkataba wa kutokomeza mabomu ya kutegwa ardhini ulianza kutumika mwaka 1999 na hadi sasa mataifa 164 yameridhia mkataba huo.