Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita vimekwisha, kwanini mabomu ya ardhini yaendelee kuleta zahma? UN

Harakati za kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini nchini Mali. (Picha:UNMAS/Marc Vaillant )

Vita vimekwisha, kwanini mabomu ya ardhini yaendelee kuleta zahma? UN

Amani na Usalama

Ingawa vita vimemaliza katika maeneo mengi duniani lakini mambomu ya kutengwa ardhini yaliyosalia yameendelea kuwa msumari wa moto juu ya kidonda kwa maelfu ya watu, yakikatili maisha yao na kuwajeruhi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe mahsusi kwa ajili ya siku ya kimataifa ya uelimishaji na msaada kuhusu mambomu ya kutegwa ardhini ambayo kila mwaka huadhimishwa Aprili 4.

Guterres amesema idadi kubwa ya mabomu hayo na vilipuzi vingine vinawaathiri maeneo yote ya yaliyokuwa na vita  na ambako vita vinaendelea mijini na vijijini na hivyo amesisitiza

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Hatua dhidi ya mabomu hayo ni muhimu sana kwani barabara zilizoondolewa mabomu na vilipuzi zinawawezesha walinda amani kufanya doria na kuwalinda raia, na endapo mashamba, shule na hospitali zikiondolewa mabomu hayo zinawezesha maisha ya watu kujerea katika hali ya kawaida. Natoa wito kwa serikali zote kutoa msaada wa kisiasa na kifedha kuruhusu kazi ya utoaji mabomu kuendelea popote inapohitajika.”

Ameongeza kuwa katika dunia ya sasa ya misukosuko hatua dhidi ya mabomu hayo ni njia muafaka ya kuelekea amani ya kudumu.  Mpango wa Umoja wa Mataifa wa huduma ya kuondoa vilipuzi na mabomu ya ardhini UNMAS unafanya kazi kubwa katika sehemu mbalimbali duniani zilizopitia au kuwa na vita ili kuondoa mabomu hayo.

Eneo la Lobonok Sudan kusini , sasa liko huru bila mabomu ya ardhini  yaliyokuwa yametapakaa mpaka hospital. Akiishukuru UNMAS kwa kuyaondoa Bi Imelda Kiden Tombe mgonjwa katika hospital ya Lobonok anasema

(SAUTI YA IMELDA KIDEN TOMBE)

“Eneo hili lilikuwa limejaa mabomu hata kuna mtu mguu wake ulipuliwa na kukatika hapa, ndio maana imetuchukua muda sana kutopita katika maeneo haya. Na sasa namshukuru Mola kwa kuwaleta kwetu wategua wamabomu hawa.”