Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Safari za ndege kuwaondoa wahamiaji kutoka Libya zarejelewa:IOM

Wahamiaji kutoka kituo walimokuwa wakishikiliwa nchini Libya na kusafirishwa hadi Niger
UNHCR/Jehad Nga
Wahamiaji kutoka kituo walimokuwa wakishikiliwa nchini Libya na kusafirishwa hadi Niger

Safari za ndege kuwaondoa wahamiaji kutoka Libya zarejelewa:IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Sitisho la mapigano lililofikiwa hiki kwenye eneo la kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli na viunga vyake limewezesha kurejea tena kwa safari za ndege za kuwarejesha nyumbani kwa hiari wahamiaji walioko  nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, wahamiaji zaidi ya 20 wameweza kuondoka kutoka Libya wakitumia  ndege ya shirika la ndege la Ghana, na hivyo kufanya iwe ndege ya kwanza kuondoka Libya kufuatia makubaliano hayo.

Hii inafuatia kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa Mitiga.

IOM inasema wahamiaji hao walitoka viunga tofauti vya mji huo  na walitaka kurejea nyumbani salama kupitia  mpango wa hiari  wa shirika  hilo wa VHR.

Kupitia mpango huo wahamiaji wanaotaka kurudi nyumbani lakini hawana njia husaidiwa na IOM kwa kuwasafirisha na punde tu wafikapo nyumbani hupewa msaada wa kuwawezesha kutulia nyumbani.

Hali ilivyo katika maeneo ya kushikilia wahamiaji na wasaka hifadhi. Hapa ni Libya nje kidogo ya mji mkuu, Tripotli.
UNICEF/Alessio Romenzi
Hali ilivyo katika maeneo ya kushikilia wahamiaji na wasaka hifadhi. Hapa ni Libya nje kidogo ya mji mkuu, Tripotli.

Mratibu wa VHR katika ofisi ya IOM nchini Libya Ashraf Hassan,amesema kuwa wamepata ahueni kidogo kurejea kwa safari hizo na wanatarajia kukodisha ndege zingine  siku zijazo ili kusafirisha wahamiaji waliosalia ambao wanataka kurejea nyumbani kwao.

Ameongeza kuwa kutokana na idadi kuongezeka, wataendelea na mpango huo wakitumia nafasi hii ya usitishwaji wa mapigano kuwasaidia warejee nyumbani salama.

 IOM imepanga safari kadhaa hapo awali lakini zikasitishwa kutokana na mapigano yaliyokuwepo majuzi mjini Tripoli, ambayo yalielezwa na mkuu wa ofisi ya IOM Libya, Othman Belbeisi, kuwa yalihatarisha maisha ya wahamiaji wengi.