Fedha za wahamiaji hukwamua nchi zao za asili- UNCTAD
Ingawa wanaishi ughaibuni, wahamiaji bado wanachangia kiuchumi kwenye nchi walizotoka. Nchi hunufaika, halikadhalika familia zao.
Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, imesema fedha zinazotumwa na wahamiaji walioko ughaibuni zimekuwa mkombozi kwa mataifa mengi ya Afrika.
Mathalani kati ya mwaka 2014 na 2016 wahamiaji walioko ughaibuni walituma jumla ya dola bilioni 65 kwa nchi za Afrika.
Afisa katika ofisi ya UNCTAD, huko Geneva, Uswisi, Jane muthumbi akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa ametaja baadhi ya nchi nufaika zaidi ikiwemo Liberia ambayo asilimia 27 ya pato la nchi hutokana na fedha zinazotumwa na wahamiaji.
Halikadhalika Gambia mwaka jana asilimia 21 ya pato la ndani na Comoro asilimia 20 ya pato la nchi lilitokana na utumwaji wa fedha.
Hata hivyo amesema kiwango kinachotumwa kingaliweza kuwa kikubwa zaidi iwapo gharama za kutuma na kupokea fedha kutoka ughaibuni ingalipunguzwa. Kwa hivyo amesema hatua muhimu ni kupunguza gharama kwa mujibu wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
Amesema kwa mujibu wa SDGs, gharama hiyo inapaswa kupunguzwa kwa asilimia 3.