Mwongozo kusaidia wakenya kutuma fedha nyumbani kwa tija

27 Agosti 2019

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM na wadau wake wanatekeleza mwongozo wenye lengo la kuwawezesa raia wa Kenya wanaoishi ughaibuni kutuma fedha nyumbani kwa njia iliyo salama zaidi na yenye tija. 

Mwongozo huo uliopatiwa jina Tuma Fedha na Wekeza Kenya, unatokana na ushirikiano kati ya serikali ya Kenya, Muungano wa Ulaya na Umoja wa nchi za Afrika, Karibea na Pasifiki pamoja na IOM kwa kuzingatia kuwa yakadiriwa kuna wakenya milioni 3 wanaoishi ughaibuni.

Akizungumzia kiwango cha fedha zinazotumwa Kenya kutoka ughaibuni, Balozi Mike Oyugi ambaye ni Mkurugenzi wa masuala ya ughaibuni katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya amesema..

(Sauti ya Balozi Mike Oyugi)

“Fedha zilizotumwa na wanaughaibuni mwaka 2018 zilikuwa shilingi bilioni 251 za Kenya. Ukilinganisha na mwaka uliotangulia wa 2017 ilikuwa shilingi bilioni 147 za Kenya na unaona kuna ongezeko la asilimia 47 kwa mwaka mmoja na hizi fedha zimekuwa zikiongezeka kila mwaka. Changamoto ni jinsi gani ya kutumia vizuri hizo fedha. Hicho ndio kitu tunashughulikia na tunataka kushirikisha wana ughaibuni ili kutatua shida zilizobainishwa na serikali.”

Mwongozo unataka mtumaji wa fedha kabla ya kutuma kuzingatia mambo manne ambayo ni mosi, kasi ya utumaji, gharama ya utumaji, usalama wa taarifa binafsi, usalama wa fedha na taratibu za mpokeaji kupata fedha,  hizo.

Kwa mantiki hiyo Balozi Oyugi amesema fedha kutoka ughaibuni ni muhimu kwa kuwa hivi sasa kiwango chake kimezidi hata mapato yatokanayo na mauzo ya mazao kama vile kahawa na chai na mboga za majani kwa hiyo lazima hatua zichukuliwe ili ziwe na mchango kwenye maendeleo ya nchi.

TAGS: Ughaibuni, wahamiaji, IOM, ACP, EU, Kenya

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud