Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yawaunga mkono wahamiaji wakati utumaji fedha duniani ukishuka kwa asilimia 20

Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa  jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote
Picha-IFAD
Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote

UN yawaunga mkono wahamiaji wakati utumaji fedha duniani ukishuka kwa asilimia 20

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakati leo ikiadhimishwa siku ya kimataifa ya utumaji fedha kwa familia , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa ombi kwa watu kila mahali kuwaunga mkono wahamiaji katika wakati huu ambapo fedha ambazo zinatumwa nyumbani kwa familia na wahamiaji hao zimepungua kwa zaidi ya dola bilioni 100 na kusababisha njaa, kushindwa kusoma, na kuzorota kwa afya kwa mamilioni ya familia duniani.

Katika ujumbe wake wa siku hii Guterres amesema anatambua dhamira ya wahamiaji milioni 200 ambao kila mara hutuma fedha nyumbani ,na familia milioni 800 katika jamii mbalimbali katika nchi zinazoendelea ambazo zinategemea fedha hizo kwa kila kitu.

Kufuatia rekodi  ya dola bilioni  554 zilizotumwa nyumbani na wahamiaji mwaka 2019, Benki ya Dunia mwezi Aprili mwaka huu ilikadiria kwamba mdororo wa kiuchumi uliosababishwa na janga la corona au COVID-19 na kusababisha sehemu nyingi kufungwa utachangia kushuka kwa kiasi kikubwa kwa kiwango cha fedha zinazotumwa nyumbani kwa takribani asilimia 19.7.

Mamilioni ya wahamiaji wamepoteza ajira na hivyo kuzisukuma familia zao zinazowategemea  kutumbukia kwenye uohehahe.

Ili kuzisaidia familia hizo,  Guterres amesema, “wahamiaji ni injini za uchumi wa dunia ambazo hutoa mchango muhimu kwa mamilioni kote duniani”.

Hivyo  Guterres ametoa wito wa kupunguzwa gharama za utumaji fedha, huduma za fedha kwa wahamiaji na familia zao hasa vijijini na kuchagiza ujumuishwaji wa kifedha kwa watu hao siku za usoni.

Wito huo unaungwa mkono na Mabelana Heri Nyanda, mmoja wa wahamiaji kutoka Tanzania anayeishi nchini Marekani ambaye yeye kilio chake ni gharama ya utumaji wa fedha akisema, kuwa "gharama za kuutuma fedha ni juu sana kwa sababu nafikiri kuna kampuni nne tu za kutuma fedha Tanzania. Kama kungalikuwepo na ushindani mkubwa hata gharama ya kutuma ingalipungua. Gharama ikiwa chini hata ukiwa na fedha kidogo unafahamu inakuwa na thamani kule tunakotuma."

Na ombi lake ni, "kuwepo na uwezekano wa kampuni nyingi zaidi za kupokea fedha kama jinsi ilivyo huko nyumbani ambako unaweza kutuma fedha kutoka na kwenda mtandao wowote wa simu. Hii itaondoka tatizo."