Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UM yuko Mali kuadhimisha siku ya walinda amani

Kamanda Olufunmilayo Ajibike Amodu wa Nigeria (kulia) kutoka Nigeria akiwa na Meja Badru Ahsan Khan, wa Bangladesh(kushoto) wote wanahudumu MINUSMA na leo wanakabidhiwa medali na Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres
Picha ya UNNews/Jerome Bernard
Kamanda Olufunmilayo Ajibike Amodu wa Nigeria (kulia) kutoka Nigeria akiwa na Meja Badru Ahsan Khan, wa Bangladesh(kushoto) wote wanahudumu MINUSMA na leo wanakabidhiwa medali na Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres

Mkuu wa UM yuko Mali kuadhimisha siku ya walinda amani

Amani na Usalama

Katika mkesha wa siku ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kesho Jumanne, polisi wa Mali wanajiandaa kwa doria za usiku kwenye barabara za mji mkuu Bamako kwa kushirikiana na walinda amani wa umoja huo

Katika mkesha wa  siku ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kesho Jumanne, polisi wa Mali wanajiandaa kwa doria za usiku kwenye barabara za mji mkuu Bamako kwa kushirikiana na walinda amani wa umoja huo.
 
Mwandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa, UN, ambaye yuko nchini humo kuripoti tukio hilo, aliweza kuandamana  na walinda amani hao kwa doria kabla ya kuwasili kwa Katibu Mkuu Antonio Guterres.
 
Guterres atakuwepo Mali kwa maadhimisho ya miaka 70 ya ulinzi wa amani wa UN unaohusisha  wanaume na wanawake waliojitolea kutumikia kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, operesheni hatari zaidi ya UN.

Image
Maafisa wa UNPOL wa kikosi cha Senegal wanapiga doria katika barabara za Gao, Mali. Picha MINUSMA / Marco Dormino

"Doria zinafanywa ili kuwahakikishia wananchi, kuwasaidia kuondokewa  na uwoga walionao kuhusu masuala ya usalama.Mwanzo wa mgogoro huu, watu walikuwa hawawezi kutoka nje kwani walikuwa wakiogopa makundi yenye silaha pamoja na mashambulizi", ameeleza Masserigne Faye, Mratibu wa kitengo cha polisi cha ujumbe huo.

Ripoti wa UN anasema kwa ujumla mji unaonekana tulivu Jumapili usiku, ambapo madereva wanakubali bila malalamiko yoyote   askari polisi kukagua  ndani ya  magari yao kama sehemu ya doria. 
 
"Ni jambo jema kwani inakufanya uwe huru kufanya kazi zako", amesema dereva wa daladala, Mamoutou Kané, baada ya kufungua mlango wa gari lake.

Souleymane Ag Alf na mkewe Makata Ag Issa wakiwa na watoto wao mapacha Fatimatou and Zenabou mjini Timbuktu, Mali, Disemba 2017.
© UNICEF/UN0156916/Dicko
Souleymane Ag Alf na mkewe Makata Ag Issa wakiwa na watoto wao mapacha Fatimatou and Zenabou mjini Timbuktu, Mali, Disemba 2017.

“Tunadhani hii inatoa hakikisho kwa wananchi.Tunataka idumu', amesema  Boubacar Traoré, akiwa amekaa nje ya kibanda katika kiunga cha  Medina Coura.
 
Siyo mji mkuu ulioko kusini mwa nchi hiyo wenye shida ya kiusalama, bali maeneo ya kaskazini na kati mwa nchi. Mali inapatikana  kaskazini magharibi mwa bara la Afrika na haina upenyo wa bahari huku  maeneo yake huingia ndani mwa jangwa la sahara.
 
Walinda amani wa kwanza wa Umoja wa Mataifa walitumwa Mali mwaka 2013 kufuatia uasi jeshini ambapo waasi walijaribu kuchukua udhibiti wa taifa hilo baada ya kutokea  mapinduzi ya kijeshi.
 
Lakini kutokana na walinda amani kuanza kulengwa na makundi yenye silaha yanayopigana dhidi ya  majeshi ya serikali ya Mali,ujumbe wa UN  sasa unakabiliwa na kazi ngumu.
 
Pamoja na kuonyesha msimamo na walinda amani, Katibu Mkuu ataonyesha mshikamo pia na waumini wa dini wa kiislamu walio kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kufunga pia yeye mwenyewe wakati wa ziara yake hii.
 
Katika ziara yake ya siku mbili, mkuu wa UN ,atakutana na vikosi vya MINUSMA pamoja na wafanyakazi wengine. Pia akiwa mjini Bamako, atakutana na rais wa Mali,  Ibrahim Boubacar Keïta na viongozi wengine waandamizi.
 
 Bwana Guterres amepangiwa kuondoka jumatano  kutoka  mji mkuu hadi mikoani kukutana na viongozi wa mikoa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wanawake, vijana na viongozi kadhaa wa kidini.