Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani 10 kutoka Chad wauawa Kidal, Mali kufuatia shambulio

Walinda amani kutoka Chad wakipiga doria katika mitaa ya Kidal nchini Mali.(maktaba Desemba 2016)
MINUSMA/Sylvain Liecht
Walinda amani kutoka Chad wakipiga doria katika mitaa ya Kidal nchini Mali.(maktaba Desemba 2016)

Walinda amani 10 kutoka Chad wauawa Kidal, Mali kufuatia shambulio

Amani na Usalama

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulizi dhidi ya kambi ya askari walinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Aguelhok, eneo la Kidal nchini Mali leo Jumapili asubuhi, ambapo askari 10 kutoka Chad wameuawa na wengine 25 wamejeruhiwa. Katika shambulio hilo, vikosi vya MINUSMA vilijibu mashambulizi na baadhi ya waasi wameuawa.

Bwana Guterres kupitia msemaji wake, ametuma salamu za rambirambi kwa serikali ya Chad na pia familia na marafiki wa marehemu, huku akiwatakia ahueni  askari majeruhi katika shambulizi hilo.

Ametambua mchango mkubwa wa walinda amani hao wanawake na wanaume kwa ujasiri wao kwa kazi zao kupitia MINUSMA, licha ya hatari zinazowakabili.

Aidha Bw. Guterres ametoa wito kwa serikali ya Mali na makundi ya wanamgambo waliosaini mkataba wa amani kufanya uchunguzi ili kubaini wahusika, na kuwachukulia hatua za kisheria haraka iwezekano.

Pia amesema, vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya askari walinda amani ni ukiukwaji wa sheria za kivita na za kimataifa. Aidha amehakikishia serikali na watu wa Mali kuwa vitendo hivyo havitaathiri juhudi za Umoja wa Mataifa katika kujenga amani na utulivu nchini humo.

Habari za UN
Kidal, Mali

 

Wakati huo huo Baraza la Usalma la Umoja wa Mataifa likilaani shambulio hilo limetuma rambi rambi zake kwa familia na wahanga, pia kwa Chad na MINUSMA. na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi.

Aidha Baraza hilo limekumbusha kuwa ugaidi katika njia yeyote ni moja ya tishio kwa amani na usalama na hivyo kusisitiza haja ya kuwawajibisha watekelezaji wa uhalifu huo.

Baraza la Usalama limerejelea  uungaji mkono mwakilishi maalum wa katibu mkuu nchini Mali na mkuu wa MINUSMA, Mahamat Saleh Annadif na vikosi vya usalama nchini Mali na ukanda wa Sahel kwa mujibu wa zimio 2423 la mwaka 2018.