Mlinda amani wa UN auawa Mali, 4 wajeruhiwa, Guterres azungumza

6 Oktoba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mashambulio mawili dhidi ya ujumbe wa umoja huo wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA ambayo yamesababisha kifocha mlinda amani mmoja huku wengine wanne wakijeruhiwa.

Habari zinasema mlinda amani huyo kutoka Chad aliuawa na wenzake watatu walijeruhiwa sana wakati msafara wao ulipokanyaga kilipuzi kwenye eneo la Aguelhok, lililoko huko Kidal kaskazini mwa Mali.

Mapema katika tukio lingine, watu wasiojulikana walishambulia kambi ya muda ya MINUSMA huko Bandiagara jimboni Mopti, katikati mwa Mali na kusababisha mlinda amani mmoja kutoka Togo kujeruhiwa.

Kupitia taarifa ya msemaji wake iliyotolewa leo jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu Guterres amesihi mamlaka za Mali pamoja na vikundi vilivyojihami ambavyo vilitia saini makubaliano ya amani yam waka 2015, wafanya juhudi zote kusaka washambuliaji ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa haraka.

Makubaliano hayo ya amani yalitiwa saini na serikali ya Mali na vikundi viwili kaskazini mwa Mali vilivyojihami kwa lengo la kumaliza mzozo ulioibuka mwaka 2012.

Halikadhalika Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mlinda amani aliyefariki dunia pamoja na serikali na wananchi wa Chad huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter