Licha ya hatari MINUSMA ina imani kwamba hatua zinaweza kupigwa kuelekea amani Mali- Gyllensporre

29 Julai 2019

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA ni muhimu sio tu kwa ajili ya taifa hilo lililopo ukanda wa Sahel au Umoja wa Mataifa bali pia kwa ajili mataifa mengi na hilo dhahiri kwa kuzingatia kuwa takriban nchi 54 zimekuja pamoja kuhakikisha kwamba zinaleta mabadiliko chanya nchini humo.

Kauli hiyo ni ya kamanda wa kikosi cha MINUSMA Jenerali  Dennis Gyllensporre katika mahojiano maalum na UN News hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Jenerali Gyllensporre amesema pamoja na umuhimu huo, operesheni hiyo nchini Mali inasalia kuwa operesheni ngumu zaidi huku ujumbe huo ukikabiliwa na changamoto ambazo kwa nadra ujumbe wa Umoja wa Mataifa haukabiliani nao huku hatari ya mabomu ya kutegwa ardhini na hatari zingine zikikabili walinda amani lakini pia raia ambao ni waathirika wakubwa.

(Sauti ya Dennis)

“Wananchi wa Mali ndio waathirika wakubwa kila siku hususan katika maeneo ya kati kati mwa nchi ambako kuna mashambulizi mengi dhidi ya raia. Tunashuhudia wanawake na watoto wakishambuliwa katika maeneo tofauti na haya ni mazingira ambayo hayakubaliki na tutafanya kila tuwezalo kukabiliana na tishio hizo.”

Hata hivyo licha ya mazingira magumu ya kufanya kazi na hatari zilizopo huku MINUSMA ikiwapoteza walinda amani wake kufuatia mashambulizi lakini Jenerali Gyllensporre amesema cha muhimu ni kujiandaa na kutotabirika kwa makundi ya waasi ambayo yanatishia usalama na kwamba wataendelea kuwepo Mali.

Aidha kamanda huyo wa MINUSMAamesema wanachohitaji ili kufanikisha hilo ni

(Sauti ya Dennis)

“Ili kupiga hatua nchini Mali kwa ujumla na ili kuimarisha usalama ni kuhakikisha kwamba serikali inaimarisha mamlaka kote nchini na kuwepo pale na kutoa huduma za kijamii ikiwemo usalama. Hiyo itakuwa njia mujarabu kurejesha nchi katika hali ya amani na uthabiti, tutakuwepo pale kutoa msaada na kuiunga mkono lakini serikali ndio mhusika mkuu katika kutatua hilo.”

MINUSMA ina walinda amani 12,644 na polisi 1,734 kutoka katika nchi mbali mbali.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter