Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO: Madaktari Gaza wanafanyakazi kutwa kucha kuokoa maisha bila kutia chochote tumboni

WHO: Madaktari Gaza wanafanyakazi kutwa kucha kuokoa maisha bila kutia chochote tumboni

Pakua

Wahudumu wa afya Gaza wanafanya kazi mchana kutwa na usiku kucha wakihaha kuokoa Maisha ya wagonjwa na majeruhi katika hospitali chache zilizosalia zikifanyakazi bila kutia chochote tumboni kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO

WHO inasema wafanyakazi hao wanaolazimika kufanyakazi saa 24 kuokoa maisha ya watu kama ambavyo wanakosa vifaa muhimu na vitendeakazi vingine vivyo hivyo wanakosa chakula cha kutosha kama ilivyo kwa maelfu mengine ya raia wa Gaza.

Timu ya WHO iliyozuru Hospitali ya Al-Aqsa katikati mwa Ukanda wa Gaza ili kupeleka vifaa muhimu imezungumza na wafanyakazi kuhusu hali zao, ikiwa ni pamoja na hali yao ya lishe.

Bashar Abdelkader, ambaye ni daktari wa kujitolea katika hospitali hiyo, amesema madaktari wanapewa chakula lakini wanakosa viambato muhimu vya lishe, hasa mchele na mboga nichache. 

Ameongeza kuwa mlo mmoja unaweza kugawiwa kwa watu wawili na zaidi ya yote,chakula haitoshi kwa daktari wa zamu wanofanyakazi kwa saa 24 hospitalini hapo.

Tahani al-Samra, ambaye pia ni daktari wa kujitolea katika hospitali ya al-Aqsa amesema "Tunakabiliwa na utapiamlo na ukosefu wa nyenzo tunazohitaji. Kwa sasa hakuna mboga za asili za majani, matunda au virutubisho vingine muhimu. Tunategemea vyakula vya makopo, ambavo bei yake inapanda kwa kasi."

WHO na washirika wake wanafanya operesheni ya hatari kubwa wakihaha kupeleka dawa, mafuta na chakula kwa wahudumu wa afya na wagonjwa. 

Lakini maombi ya ufikishaji wa bidhaa mara nyingi hukataliwa au kutatizwa. Uharibifu wa barabara na mapigano yanayoendelea, ikiwa ni pamoja na ndani na karibu na hospitali, pia yanatatiza utoaji wa misaada.

WHO imeonya kwamba bila kuwepo hatua kubwa na za haraka za utoaji wa chakula, maji na vifaa vya msingi, hali ya Gaza, ambako njaa inaathiri karibu watu wote, karibu familia zote zinalazimika kuruka mlo kila siku na watu wazima wanapunguza kiwango cha ulaji wao wa kula.

Nusu ya watu wote ambao ni  watu milioni 1.1 huko Gaza, wamechoka kabisa na hakuna usambazaji wa chakula na uwezo wao wa kukabiliana na njaa mbaya ni mdogo. 

Umoja wa Mataifa unasema “Hii ndiyo idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika orodha ya watu wanaokabiliwa na njaa kali Gaza.”

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'32"
Photo Credit
© WHO