Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP/UNICEF: Janga kubwa la njaa duniani linanyemelea Sudan miezi 11 baada ya kuzuka vita

WFP/UNICEF: Janga kubwa la njaa duniani linanyemelea Sudan miezi 11 baada ya kuzuka vita

Pakua

Takriban miezi 11 tangu majenerali wapinzani watangaze vita nchini Sudan, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa leo walionya kwamba mzozo huo unaweza kusababisha janga kubwa zaidi la njaa duniani. 

Sudan, nchi iliyo kaskazini mashariki mwa Afrika tayari iko katika mzozo mkubwa zaidi wa watu waliofuriushwa makwao duniani kwa mujibu, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP.

Na mapigano yanayoendelea kati ya Jeshi la Sudan SAF na kundi hasimu la msaada wa haraka RSF yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine milioni nane kuyahama makazi yao ndani ya nchi na wengine kukimbilia nchi jirani.

Hivi sasa watoto milioni 14 wanahitaji haraka msaada wa kuokoa maisha, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF katika tahadhari yale ya hivi karibuni, huku kukiwa na wasiwasi kwamba mzozo huo unaweza kuenea kwenye mipaka ya Sudan, na kutishia maisha na amani katika eneo hilo, endapo mapigano hayo hayatokoma.

Cindy McCain, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa WFP amesema "Miaka ishirini iliyopita, Darfur ilikuwa janga kubwa zaidi la njaa duniani na ulimwengu ulijitolea kuchukua hatua. Lakini leo hii watu wa Sudan wamesahaulika. Mamilioni ya maisha ya watu, amani na utulivu wa eneo zima viko hatarini,” 

Bi. McCain ameyasema hayo akiwa Sudan Kusini, ambako amekutana na familia zilizokimbia ghasia na hali mbaya ya njaa Sudan na kuingia hiyo jirani zao. 

Amesema hivi sasa WFP inahaha kutimiza mahitaji ya chakula na kuongeza kuwa "Nimekutana na kina mama na watoto ambao wamekimbia Sudan ili kuokoa maisha yao sio mara moja, lakini mara nyingi, na sasa njaa inawanyemelea. Madhara ya kutochukua hatua yanakwenda mbali zaidi ya mama kushindwa kulisha mtoto wake na yataathili eneo hilo kwa miaka mingi ijayo”.

WFP inasema leo hii chini ya mtu mmoja kati ya 20 Sudan ndiye anayeweza kumudu kupata chakula, watu 9 kati ya 10 wanakabiliwa na njaa  na mgogoro wa chakula umesambaa hadi nchi jirani zinazohifadhi wakimbizi wa Sudan na kuathiri watu zaidi ya milioni 25 Sudan, Sudan Kusini, na Chad.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'32"
Photo Credit
© WFP/Hugh Rutherford