Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

22 FEBRUARI 2024

22 FEBRUARI 2024

Pakua

Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina, ambapo FAO limeutenga mwaka huu wa 2024 kuwa wa wanyama wa jamii ya ngamia kwani mchango na faida zake zinanufaisha zaidi ya mataifa 90 duniani na tunaelekea nchini Kenya kwa makala inayohusu ngamia. Pia tunaangazia DR Congo, Gaza na Ukraine kwa muhtasari ya habari. Katika kujifunza kiswahili tunakuletea uchambuzi wa neno “NDONGOSA”.

  1. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) kwa kushirikiana na wadau wake 105 hii leo wamezindua mpango wa kuwasaidia wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, DRC pamoja na jamii zilizowakaribisha. Mpango huo uliozinduliwa hii leo jijini Pretoria, Afrika Kusini utakaogharimu jumla ya dola milioni 668 kwa kipindi cha mwaka 2024-2025 unahusisha wadau kutoka Tanzania, Burundi, Uganda, Rwanda, Angola, Zambia na DRC yenyewe.
  2. Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA Philippe Lazzarini na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani Dkt. Tedros Ghebreyesus wakiunga mkono tamko la Kamati ya kudumu ya mashirika ya kimataifa (IASC) lililotolewa jana kuhimiza kusitiza mapigano Gaza, kupitia kurasa zao za mtandao wa X wameeleza hali ilivyo tete Gaza. Lazzarini akihoji ni “mara ngapi zaidi tunapaswa kukumbusha kwamba hakuna mahali salama katika Gaza?”  huku Dkt. Tedros akieleza kuwa hospitali zimegeuka uwanja wa vita. 
  3. Na Uvamizi kamili wa Ukraine uliofanywa na Urusi ukielekea kuingia mwaka wa tatu, Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametoa wito kwa Urusi kuruhusu Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu na mashirika mengine huru ya kimataifa kuwafikia kikamilifu wale wote ambao wamenyimwa uhuru wao katika muktadha wa vita ya kijeshi. Wakati huo huo nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limeeleza kuwa asilimia 40 ya idadi ya watu wote wa Ukraine bado wanahitaji aina fulani ya usaidizi wa kibinadamu, wakati wakimbizi milioni 2.2 wanahitaji msaada katika nchi za jirani.
  4. Katika kujifunza lugha ya Kiswahili leo ukumbi ni wake mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA anafafanua maana ya neno “NDONGOSA”.

Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
11'55"