Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

16 NOVEMBA 2023

16 NOVEMBA 2023

Pakua

Hii leo jaridani mada kwa kina ambapo ulimwengu ukijiandaa kuadhimisha siku 16 za harakati kukabiliana na ukatili wa kijinsia katika jamii zinazoendeshwa na Umoja wa Mataifa, baadhi ya sehemu duniani zimeanza kulipa suala Hilo uzito mkubwa ikiwemo Kenya. Kwa ushirikiano wa Shirika la Umoja wa mataifa la masuala ya wanawake UN Women na mengine yasiyo ya kiserikali, Kaunti ya Kakamega nchini nchini humo imefanikiwa kuzindua mpango maalum wa kuwapa waathirika wa ukatili wa kijinsia huduma za mahakamani pasi na malipo. UN Women imewashika mkono baadhi ya walioathirika kwa kuwapa bidhaa za matumizi na pia mtaji kuwawezesha kuanza biashara baada ya kuondoka kwenye vituo salama na vya Staha. Pia tunakuletea habari kwa ufupi zikiwemo kutoka Gaza, Ethiopia n aza WHO kuhusu matumizi ya tumbaku. Katika kujifunza Kiswahili leo tunabisha hodi Chuo Kikuu cha Zetech Limuru nchini Kenya kuchambuliwa maana ya Methali “Ukilima Pantosha utavuna pankwisha”. 

  1. Kamishina Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) Philippe Lazzarini kupitia ukurasa wake wa X ameandika "Kila siku ni siku ya huzuni kwa Umoja wa Mataifa na UNRWA, na kwamba anasikitika kuthibitisha kwamba wenzake 103 wameuawa Gaza tangu 7 Oktoba. Naye Tom White, Mkurugenzi wa UNRWA Gaza pia kupitia X ameandika kukosekana kwa mafuta inamaanisha ukosefu wa maji ya kunywa na kusababisha ongezeko la asilimia 40 la ugonjwa wa kuhara kwa watu wanaojihifadhi katika shule. Wakati ho huo Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk akisisitiza kuwa njia ya kisiasa inahitajika kuitoa Gaza kwenye janga la kibinadamu. 
  2. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO), leo limezindua rasmi kampeni ya "Acha uwongo" ikiwa ni hatua muhimu ya kuwalinda vijana dhidi ya sekta ya tumbaku na bidhaa zao. WHO inasema Sekta ya tumbaku ina historia ndefu ya kusema uwongo kwa umma, hata kufikia kusisitiza kwamba uvutaji sigara hausababishi saratani ya mapafu. Pia sekta hiyo inaendelea kutumia njia tofauti kueneza habari potofu, ikijumuisha kupitia watu maarufu katika mitandao ya kijamii, kufadhili matukio, na hata kufadhili wanasayansi na utafiti wenye upendeleo.
  3. Na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema linafufua mfumo wake ulioboreshwa wa operesheni nchini Ethiopia, hatua kubwa ambayo itaanza kuwafikia watu milioni 3.2 kwa msaada wa chakula kwa mara ya kwanza tangu Juni 2023. Msaada wa chakula wa WFP ulisitishwa nchini kote Ethiopia kufuatia ripoti za uporaji wa misaada.
  4. Katika kujifunza lugha ya Kiswahili mtaalam wetu leo ni Nicholus Makanji mhadhiri katika chuo Kikuu cha Zetech Limuru Kenya akitufafanulia maana ya methali “Ukilima Pantosha utavuna pankwisha.” 

Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
12'2"