Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watoto bado wanaishi kwenye maji machafu yaliyotwama nchini Pakistan - UNICEF

Mamilioni ya watoto bado wanaishi kwenye maji machafu yaliyotwama nchini Pakistan - UNICEF

Pakua

Nchini Pakistani, janga la uhai wa mtoto bado ni changamoto kubwa kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko zaidi ya miezi minne iliyopita huku idadi ya maambukizi  ya magonjwa ya hewa na utapiamlo uliokithiri au unyafuzi ikiendelea kuongezeka, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF wakati huu ambapo jumuiya ya kimataifa inajiandaa kwa ajili ya mkutano wa kuchangia taifa hilo la Asia ili lijenge mnepo dhidi ya majanga.

Miezi minne na nusu tangu kutangazwa kwa hali ya dharura kutokana na mafuriko makubwa yaliyokumba Pakistan kuanzia mwaka jana, bado  watoto milioni 4 wanaoishi karibu au kwenye maji ya mafuriko  yaliyotwama wanakumbwa na zahma na hivyo kutishia uhai na ustawi wao. 

UNICEF kupitia taarifa iliyotolewa huko Islamabad, Pakistan inasema maambukizi makali ya magonjwa ya njia ya hewayameongezeka kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko, bila kusahau unyafuzi ambapo takribani watoto milioni 1.5 wanahitaji lishe ya kukabiliana na unyafuzi ili kuokoa maisha yao. 

Mwakilishi wa UNICEF nchini Pakistan, Abdullah Fadil amesema watoto wanaoishi kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko wametumbukia zaidi kwenye majanga akisema, “mvua imekoma lakini janga kwa watoto bado limechachamaa.” 

Huko Jacobabad, wilaya ya kusini mwa Paksitan ambako familia hazina zaidi ya kitambaa kufunika makazi yao yaliyotwama kwenye maji, viwango vya joto nyakati za usiku vinashuka hadi nyuzijoto 7 katika kipimo cha Selsiyasi. 

Video ya UNICEF inaonesha mkuu wake wa ofisi ya mashinani jimboni Sindh huko Jacobabad, akisambaza vifaa vya kutia joto ikiwemo blanketi ambapo watu 200,000 wakiwemo watoto, wanawake na wanaume wamenufaika na miongoni mwa watoto wanufaika anatabasamu. 

Msaada pia ni wa huduma za lishe, chanjo dhidi ya Polio na huduma za maji safi na salama, bila kusahau vikasha vya kujisafi kwa watu milioni moja. 

Pamoja na kutoa huduma hizo UNICEF inaendelea kurejesha huduma muhimu za afya, kujisafi na elimu kwenye maeneo yaliyoathirika ili wanaorejea makwao waweze kuendelea na maisha. 

Hata hivyo UNICEF inasema ili iweze kukamilisha operesheni zake kwa ufanisi, jamii ya kimataifa iongeze usaidizi wake kwa kutoa fedha kwa wakati. 

Ombi la sasa la UNICEF kufanikisha operesheni zake za kusaidia wanawake na watoto walioathiriwa na mafuriko Pakistani ni dola milioni 173.5 lakini limefadhiliwa kwa asilimia 37 pekee. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'29"
Photo Credit
© UNICEF/Asad Zaidi