Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS imewajengea shule wakazi wa Mvolo Sudan Kusini

UNMISS imewajengea shule wakazi wa Mvolo Sudan Kusini

Shule hii itawasaidia watoto wetu kuepuka mimba zisizotarajiwa na kuzurura mitaani:Jenty Elisa

Mpango wa Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS umeleta nuru kwa wananchi wa eneo la Mvolo jimbo la Equatorial Magharibi kwa kuwajengea shule na kituo cha polisi hatua ambayo wananchi wanasema etaepusha zahma nyingi kwa watoto wao. Evarist Mapes ana taarifa zaidi

(TAARIFA YA EVARIST MAPESA)

Natts…Jenty Elisa

Huyo ni mkazi wa Mvolo Jenty Elisa akisema kwa furaha kubwa sasa watawachagiza watoto wao wavulana na wasichana kujiunga na shule na kuepuka kuzurura hovyo na hawa watu wazima kujiunga na elimu ya ngumbaru.

Kauli yake inafuatia hatua ya UNMISS kujenga kituo cha polisi na shule iliyokuwa ikihitajika kwa muda mrefu katika eneo hili linalopakana na jimbo la Lakes ambalo limeathirika vibaya na mgogoro wa Sudan Kusini na linaendelea kushuhudia mivutano ya kijamii na wizi wa ng’ombe ambao umewalazimisha watu wengi kuzikimbia nyumba zao na kutelekeza mashamba yao.

Japo hivi sasa taratibu maisha yameanza kurejea katika hali ya kawaida kutokana na kupungua kwa mizozo lakini bado kuna changamoto kama vile za elimu na huduma za afya.

Hivyo UNMIS imeamua kuchukua hatua kwa kuwajengea shule jamii hii ili kuchangia ujenzi wa amani kwa kikazi hiki na kijacho na pia kuichagiza jamii iliyokimbia kurejea nyumbani. Moses Bagari ni afisa wa UNMISS wa ulinzi kwa watoto anasema

“Wakati wa doria zetu tunapokuja hapa hatufanyi tu doria na kuondoka, lakini pia tunaona changamoto. Tunaona changamoto za watoto kusomea chini ya miti, na hivyo tukalizingatia hilo wakati wa mizunguko yet una kusema kwanini tusifanye kitu ili kiwape watoto mazingira mazuri ya kupata elimu na kujifunza hivyo tulitoa mapendekezo na yakafanyikiwa. Na hiyo ni moja ya haki za msingi za watoto kupata fursa ya elimu.”

Kwa wazazi kama Jenty Elisa ambaye ni mkazi wa Mvolo ujenzi huo wa shule anasema unatoa zaidi ya fursa ya elimu kwani

(SAUTI YA JENTY ELISA-FLORA)

“Watoto wetu wamkuwa wakipata wamekuwa wakipata mimba zisizotarajiwa kutokana na ukosefu wa shule. Hata wavulana baada ya kumaliza elimu ya msingi darasa la 8 huo ndio unakuwa ukomo kwani hatuna shule za sekondari hapa. Leo niña furaha sana kwamba tumejengewa na kukabidhiwa shule ya sekondari.”

Mbali ya shule UNMISS pia imejenga kituo cha polisi katika eneo hilo ili kupunguza uhalifu na kuimarisha utawala wa sheria.

TAGS:UNMISS, Sudan Kusini, Elimu, shule, Mvolo, kituo cha polisi

 

 

Pakua
Audio Credit
UN News/ Evaristi Mapesa(Radio partner)
Photo Credit
UNMISS