Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utoaji chanjo kwa watoto duniani warudi nyuma, ingawa Uganda imekuwa imara- Ripoti

Utoaji chanjo kwa watoto duniani warudi nyuma, ingawa Uganda imekuwa imara- Ripoti

Pakua

Licha ya mwaka 2021 kutegemewa utakuwa mwaka bora wa utoaji chanjo kwa watoto wachanga baada ya janga la COVID-19 kuvuruga utoaji chanjo mwaka 2019 na 2020, ripoti iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa imeonyesha kiwango cha utoaji chanjo duniani kimeendelea kupungua mara dufu na kurudisha takwimu kwa miongo mitatu nyuma huku watoto milioni 25 wakikosa chanjo muhimu za kuokoa maisha yao. Leah Mushi ametuandalia taarifa zaidi

Ripoti hiyo ya pamoja iliyotolewa leo jijini New York, MArekani na GEneva Uswisi na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la Afya duniani WHO na la kuhudumia Watoto UNICEF  imeeleza kuwa utoaji wa chanjo dhidi ya dondakoo, pepopunda, kifaduro ulishuka kwa asilimia tano mwaka 2019 na mwaka 2021 imeshuka hadi asilimia 81.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell ameonya kuwa ripoti hiyo ni” tahadhari nyekundu juu ya afya ya Watoto “hata hivyo amesema hatari hiyo kubwa inaweza kuzuilika.

“Janga la covid-19 sio sababu tena ya kutotoa chanjo na bado tunashuhudia utoaji chanjo ukishuka. Tunapaswa kuhakikisha kuna upatikanaji wa chanjo kwa mamilioni ya watoto waliokosa chanjo hizo la sivyo tutashuhudia mlipuko zaidi wa magonjwa, watoto wengi wata ugua na hii itaongeza shinikizo kubwa katika mifumo ya afya ambayo kwasasa tayari ipo kwenye matatizo.”

Miongoni mwa sababu za ongezeko la watoto kutopata chanjo ni pamoja na kuongezeka kwa watoto wanaoishi kwenye maeneo yenye mapigano au mazingira hatarishi kiusalama ambayo ufikishaji wa chanjo umekuwa changamoto, kuongezeka kwa taarifa za uongo na upotoshaji kuhusu chanjo pamoja na changamoto nyingine zilizosababishwa na janga la COVID-.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema nchi zinapaswa kuhakikisha zinajipanga vyema na kuhakikisha kila eneo katika sekta ya afya linaguswa

“Tunapopanga kupambana na COVID-19 tunapaswa pia kwenda sambamba na mipango ya utoaji chanjo ya magonjwa kama surau, nimonia na kuhara. Hapa sio swali la twende na hii au hii”.

Hata hivyo ripoti hiyo imesifu nchi za Uganda na Pakistan kwa kuwa na mipango madhubuti wakati wakishughulikia janga la COVID-19 ambapo walijumuisha pia utoaji chanjo kwa watoto.

Nchi zilizoathirika zaidi kwenye kushindwa kufikia idadi kubwa ya watoto kuwapatia chanjo ni zile za kipato cha chini na cha kati ambazo ni India, Nigeria, Indonesia, Ethiopia na Ufilipino na zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watoto ambao hawajapata chanjo. 

Nchi nyingine ambazo mwaka 2021 watoto wengi walikosa chanjo ni Myanmar na Msumbiji.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
2'51"
Photo Credit
© UNICEF/UN0624023/