Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

31 Mei 2022

31 Mei 2022

Pakua

Jaridani Jumanne Mei 31, 2022 na Leah Mushi-

HABARI KWA UFUPI

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO leo limetoa taarifa mpya kuhusu kiwango ambacho tumbaku inaharibu mazingira na afya ya binadamu, ikitaka hatua zichukuliwe ili kuifanya sekta hiyo kuwajibikia zaidi juu ya uharibifu inayosababisha.

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya tumbaku, WHO imesema,kila mwaka sekta ya tumbaku hugharimu dunia zaidi ya maisha ya watu  milioni 8, miti milioni 600, ekari 200,000 za ardhi, tani bilioni 22 za maji na tani milioni 84 za hewa ukaa.

Nyingi ya tumbaku hulimwa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, ambapo maji na mashamba mara nyingi yanahitajika zaidi kuzalisha chakula kwa ajili ya kanda. Badala yake, yanatumiwa kukuza mimea hatari ya tumbaku, huku misitu mingi ikikatwa miti kwa ajili ya upanzi.

 

Zaidi ya watu milioni 30 walikimbia makazi yao kutokana na majanga mwaka 2020 pekee, na idadi hii huenda ikaongezeka kutokana na kuongezeka kwa hatari na idadi ya matukio makubwa yanayohusiana na hali ya hewa. Jopo katika Kikao cha 7 cha Jukwaa la Kimataifa la Kupunguza Hatari za majanga (GPDR2022), lililosimamiwa na Sarah Charles, Msimamizi Msaidizi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani, limeangazia mbinu za kuimarisha utawala ili kupunguza hatari za majanga ya kuhamishwa.

Baadhi ya wanajopo walijadili kuwa kujihusisha na jamii zilizoathiriwa ni muhimu, haswa katika kesi za mataifa ya visiwa vidogo na jamii ya watu wa asili.

Hindou Oumarou Ibrahim, Rais wa Chama cha Wanawake wa jamii ya asili na Watu wa Chad, alisema kuwa kuenea kwa jangwa kunaleta tishio lililopo kwa jamii asilia na vijijini. "Katika kipindi cha miaka 50 tu tutakuwa na jangwa katikati ya mji wangu, N'Djamena," alisema, ambayo inamaanisha kupoteza upatikanaji wa chakula, na malisho na maji kwa ajili ya ng'ombe.

"Tunapoteza nyumba yetu kwa uharibifu wa mfumo wa ikolojia, ni sehemu yetu, ni sehemu ya utambulisho wetu, utamaduni wetu."Amesema Bi Ibrahim.

===========================================

Na Juhudi zinazofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO za kusaka misaada kwa ajili ya wananchi wa Sudan wanaokabiliwa na njaa, ukame, na hali ngumu ya maisha ambayo kwa ujumla imechochewa na vita ya Ukraine zimezaa matunda baada ya mradi wao mpya kupata ufadhili wa dola milioni 12 kutoka Mfuko wa kukabiliana na dharura wa Umoja wa Mataifa CERF.

FAO imetangaza leo kupokea msaada huo wa fedha ambao utasaidia kaya laki moja na themanini elfu au wananchi laki 9 ambao ni wakulima, wafugaji kutoka kaunti 14 za nchi hiyo zilizoathirika zaidi, wakimbizi wa ndani, wakimbizi waliorejea, wakimbizi na wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini.

Mwakilishi wa FAO nchini Sudan Babagana Ahmadu amesema  “Mchango huu wa ukarimu kutoka kwa CERF unamaanisha kuwa FAO inaweza kutoa kwa haraka pembejeo muhimu za kilimo kwa kaya za wakulima zilizo hatarini kabla ya msimu mkuu wa kilimo kuanza mwezi Juni. Itahakikisha kwamba wanaweza kuzalisha chakula cha kutosha kukidhi mahitaji yao kwa miezi ijayo.”

Takwimu za FAO zimebainisha kuwa takriban watu milioni 11 au asilimia 3 ya wananchi wa Sudan wanategemea msaada wa kibinadamu ili kuendesha maisha yao hii ikiwa ni idadi kubwa zaidi katika kipindi cha muongo mmoja.

Katika mada kwa kina tunaelekea Geneva Uswis ambako mkutano wa baraza la afya duniani umefunga pazia mwishoni mwa wiki, tutamsikia Waziri wa afya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeongoza ujumbe wa taifa hilo kwenye mkutano huo wa kimataifa.

Na mashinani ni ujumbe wa Kapteni Abdallah Kikondo Mohamed, ambaye ni Ofisa wa Intelijensia wa Kikosi cha 9 cha Tanzania, TANZBATT 9, kinacholinda amani chini ya Ujumbe wa Umoja wa mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO.

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
13'16"