Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyongeza ya dola milioni 40 kusaidia DRC kukabili dharura za kiafya ikiwemo Ebola

Nyongeza ya dola milioni 40 kusaidia DRC kukabili dharura za kiafya ikiwemo Ebola

Pakua

Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 40 kwa ajili ya kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ikabiliane na dharura za kiafya zinazokabili taifa hilo, ikiwemo ugonjwa wa Ebola na Surua. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

Katika shule ya Ikenge katikati mwa mji wa Mbandaka jimboni, Equateur nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wanafunzi wakinawa mikono, moja ya kanuni za kujikinga na Ebola. Katika eneo hilo Ebola imepiga kambi muda mrefu ikitoweka na kurejea.

Ni kutokana na hali hiyo na kwa kuzingatia dharura za kiafya ambazo DRC inapambana nazo hivi sasa ikiwemo ugonwa wa Surua na janga la Corona au COVID, 19, mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya dharura, OCHA,  Mark Lowcock ametoa fungu hilo la fedha punde baada ya DRC kuthibitisha mlipuko mpya wa Ebola mjini Mbandaka.

Taarifa ya OCHA iliyotolewa jijini New York, Marekani leo inasema kuwa DRC inakabiliana na mlipuko wa muda mrefu wa Ebola ambao tangu uanze tena mwezi Agosti mwaka 2018, umesababisha vifo vya watu 2,200 huko jimboni Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Bwana Lowcock anasema kuwa, “fedha za CERF zitaimarisha huduma za afya za sasa hivi DRC na kuwezesha ufuatiliaji wa manusura wa Ebola na kuanzisha mfumo wa kijamii wa ufuatiliaji, utoaji taarifa mapema na uchukuaji hatua kwenye ngazi ya jamii. Halikadhalika zitasaidia kulipia vyakula, maji, huduma za kujisafi , afya na elimu pamoja na ulinzi.”

Mkuu huyo wa OCHA anasema kuwa, “kile kinachoendelea DRC kinakumbusha kuwa jamii ya kimataifa haipaswi kusahau majanga ya kibinadamu ambayo yalikuwepo kabla ya janga la Corona. Iwapo tutafumbia macho maeneo kama vile DRC, watu walio hatarini ambao wamenasa kwenye mzunguko wa machungu hawatakuwa na fursa ya kukabili janga la COVID-19.”

Kwa mwaka huu, mara kadhaa DRC imekuwa katika hatua za mwisho za kutokomeza Ebola, lakini kisha ugonjwa unaibuka tena.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, linapendekeza kusubiri siku 42 baada ya mgonjwa wa mwisho kupimwa kwa mara mbili na kubainika hana Ebola, kabla ya kutangaza kutokomezwa kwa ugonjwa huo.

OCHA inasema kuwa juhudi endelevu zinahitajika kuepusha kuibuka kwa magonjwa ikiwemo kujengea uwezo harakati dhidi ya Ebola wakati wa mlipuko na kuimarisha mifumo ya afya kwa mujibu wa mipango ya serikali ya huduma ya afya kwa wote.

Fedha zilizotolewa leo ni nyongeza ya fungu la dola milioni 30 zilizotolewa awali na CERF.

Audio Duration
2'25"
Photo Credit
UN Photo/Martine Perret