Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimae misaada ya kibnadamu imefika Ghouta-WFP

Hatimae misaada ya kibnadamu imefika Ghouta-WFP

Msaada wa kibinadamu kwa eneo la Ghouta mashariki kiunga cha mji mkuu wa Damascus hatimae umeingia eneo hilo. Hii ni kwa mujibu wa ujumbe wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP kupitia ujumbe wake  wamtandao wa  kijamii wa twitter.

Twitter hiyo ya WFP ina picha ikionyesha magari ya WFP yakiwa njiani katika  safari ambayo ujumbe mtandaoni unasema kuwa ndio wameingia Ghouta. Msafara huo unapeleka msaada wa chakula pamoja na msaada mwingine kwa watu takriban elf 27 na nusu.

Mwishoni mwa juma Umoja wa Mataifa  ulimesema kuwa uko tayari kupeleka msaada Ghouta mashariki  siku ya leo jumatatu.

Umoja wa Mataifa ulisema kuwa msaada huo utapelekwa na magari 46 yakiwa yamebeba shehena za msaada wa lishe na vifaa vya afya.

Mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Syria na wakati huohuo akiwa mjumbe mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Ali Al-Za’tari jana alikuwa amesema  kuwa kikosi chake kilikuwa tayari kwa kazi hiyo.

Eneo la Ghouta -mashariki lilielezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonnio Guterees kama -jahanamu duniani, limekuwa chini ya mzingiro na majeshi ya serikali kwa muda mrefu na lina  takriban watu 400,000.

Febuari 24, baraza la usalama la Umoja wa mataifa lilipitisha, kwa kauli moja ,azimio la kuwepo usitishwaji wa mapigano wa siku 30 nchini kote Syria, kama nyongeza kwa  hatua zingine za kuondoa mizingiro sana sana Ghouta -mashariki.

Shirika la misaada la Umoja wa mataifa la OCHA limeripoti kuwa UN pamoja na washirika wake wamepokea ruksa wa kupeleka misaada kusaidia watu 70,000 mjini Duma na kuongeza kuwa  misaada iliyosalia itapelekwa huko machi nane, hii ni kwa mujibu wa  taarifa iliyotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa.

Pakua
Audio Credit
John Kibego
Audio Duration
1'30"
Photo Credit
Picha:WFP