Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa wa malaria na harakati za kuutokomeza

Ugonjwa wa malaria na harakati za kuutokomeza

Pakua

Malaria, ni ugonjwa ambao bado unaendelea kutishia maisha ya nusu ya watu ulimwenguni kote. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya ulimwenguni WHO, bara la Afrika ndio linaloongoza kwa visa vya malaria kwa asilimia 90, hususan kusini mwa jangwa la Sahara ambalo linabeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huo.

Tarehe 25 mwezi Aprili kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya malaria, lengo ni  kutokomeza gonjwa hilo.

Mwaka 2015, kulikuwa na takribani visa milioni 212 vya malaria na takribani vifo 429,000 ulimwenguni kote, watoto chini ya umri wa miaka mitano wakiwa ni waathirika zaidi. Katika mwaka huo pekee, ulimwenguni kote, Malaria imepora maisha ya watoto 303,000 chini ya miaka mitano, kati yao 292,000 kutoka bara la Afrika, sawa na kifo cha mtoto mmoja kila dakika mbili.

Katika kuadhimisha siku ya malaria duniani mwaka huu, yenye maudhui ya “Tokomeza Malaria Kabisa”, WHO inamulika mafanikio ya hivi karibuni yanayoonyesha kuwa kuzuia kunafanya kazi. Mikakati iliyowekwa na shirika hilo  kuzuia na kudhibiti ugonjwa huo tangu mwaka 2010 imepunguza visa vya malaria kwa asilimia 29% ulimwenguni kote. Mwaka huu, WHO imetoa mwongozo mpya ikipendekeza zana za kupambana na malaria katika miaka miwili ijayo, na lengo kuu ni kuutokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2020.

Photo Credit
Mama mwenye tabasamu tosha akiwa na mwanae akisimama ndani ya neti huko Arusha, Tanzania.(Picha:©UNICEF/PFPG2014-1191/Hallahan)