Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Chanjo zinahitajika haraka ili kuzuia magonjwa ya mlipuko

Mwanamke akihudhuria kliniki ya afya akiwa na mtoto mchanga katika Ukanda wa Gaza.
© UNRWA
Mwanamke akihudhuria kliniki ya afya akiwa na mtoto mchanga katika Ukanda wa Gaza.

Gaza: Chanjo zinahitajika haraka ili kuzuia magonjwa ya mlipuko

Afya

Katika jitihada za kuzuia janga la ugonjwa wa polio huko Gaza, Mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa hii leo walirudia wito wao kwa jumuiya ya kimataifa wa kusitishwa kwa mapigano ili kuruhusu kampeni kubwa ya utoaji chanjo kuanza.

Takriban miezi 10 ya vita na mashambulizi makali ya Israel yamesambaratisha huduma ya afya huko Gaza na kuvuruga mzunguko wa kawaida wa utoaji chanjo kwa watoto, na kuwaacha wakiwa kwenye hatari ya kupata magonjwa mbalimbali yanayoweza kuzuilika ikiwemo polio, ambayo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) lilithibitisha kuwepo kwa wagonjwa mwezi uliopita. Kotoka kwenye sampuli kadhaa za maji taka zilizochukuliwa kutoka Gaza.

Wito wa kuhakikishiwa usalama

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo, msemaji wa WHO Christian Lindmeier alisema kuwa usitishaji mapigano utakuwa suluhisho "bora zaidi", kabla ya kutoa wito angalau kwa barabara za eneo hilo kuwekwa wazi na kusaidia upatikanaji salama wa matibabu na vifaa vingine vya msaada viweze kupita.

"Vinginevyo, chanjo zingekuwa zimnapatikana lakini hilo halijawezekana kwakuwa malori mengi yapo nje ya mpaka, ama kwa upande wa Rafah au katika vituo vingine vya ukaguzi ama ndani ... au nje ya Gaza," alisema Lindmeier ikiwa ni wiki moja tangu shirika lao litangaze kuwa linatuma chanjo milioni moja za polio kwenda Ukanda wa Gaza.

Hakuna wagonjwa wa kupooza walioripotiwa hadi kufikia sasa, kwa mujibu wa WHO.

Naye msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) James Elder amesema ikiwa mtoto atapokea dozi kamili ya chanjo, hatari ya kuambukizwa polio ya kupooza itapotea.

Amesisitiza kuwa viwango vya chanjo vilikuwa "juu sana" kabla ya vita kuzuka kutokana na mashambulizi yanayoongozwa na Hamas kwenye maeneo mengi kusini mwa Israel ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,250 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka. "Lakini kuhamishwa kwa watu wengi, uharibifu wa miundombinu ya afya, mazingira ya utendakazi yasiyo salama, yote haya yanafanya kuwa ngumu zaidi, na hivyo kuwaweka watoto zaidi hatarini," alisema, akiongeza kuwa chanjo sasa iko karibu asilimia 89 - "kwa hivyo hatari kwa watoto imeongezeka".

Maji yamesalia kuwa haba katika Ukanda wa Gaza.
© UNRWA
Maji yamesalia kuwa haba katika Ukanda wa Gaza.

Dharura ya maji

Akilaani uharibifu ulioripotiwa wiki iliyopita wa kituo kikuu cha kutibu maji katika mji wa kusini wa Rafah, Elder alisisitiza hatari za kiafya ambazo zilizua kwa Wanagaza, sasa kwamba "Kimelipuliwa ... Ni ukumbusho mwingine mbaya wa mashambulizi haya kwa familia ambazo tayari zinahitaji maji,” alisema.

Leo kote Gaza, wastani wa upatikanaji wa maji umeshuka hadi kati ya lita mbili na tisa kwa kila mtu, kwa siku, ambapo kiwango cha chini kinapaswa kuwa lita 15, Elder aliendelea. "Kwa namna fulani watu wanahimili hivyo hivyo, lakini bila shaka sasa tuko katika mzunguko huo wa vifo ambapo watoto wana utapiamlo, kuna joto kali, ukosefu wa maji, kuna ukosefu wa vyoo wa kutisha na huo ndio mzunguko. Zaidi ya yote hayo, bila shaka, kuna mzozo mkubwa sana.”

Homa ya Ini

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA linasema watoto wengi zaidi kwenye eneo hilo wako hatarini kuambukizwa ugonjwa wa homa ya ini aina ya A kutokana na mlundikano wa watu kwenye makazi, ukosefu wa maji safi, sabuni na vifaa vingine vya kujisafi. UNRWA inasema miezi 10 ya vita imeweka mazingira rafiki kwa ugonjwa huo na mengine kushamiri na kutishia uhai wa watoto.

Shirika hilo linakadiria idadi ya wagonjwa wa homa ya ini aina ya A huko Gaza wameongezeka kwa takriban 40,000 tangu kuanza kwa vita na watoto wengi wapo hatarini kupata ugonjwa huo kutokana na kuhamishwa mara kwa mara, mlundikano wa watu katika makazi ya wakimbizi, ukosefu wa maji safi na huduma za kujisafi.

Huko Khan Younis, maelfu ya watu wanakimbia kuokoa maisha yao tena.
© UNRWA
Huko Khan Younis, maelfu ya watu wanakimbia kuokoa maisha yao tena.

Taka ngumu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP limetaka hatua za haraka zichukuliwe katika kudhibiti taka ngumu.

Kulingana na tathmini mpya iliyofanywa na shirika hilo, hakuna ufikiaji wa dampo kubwa, na taka hujilimbikiza katika maeneo zaidi ya 140 ya kutupa taka ambayo husababisha hatari kubwa za kiafya na mazingira, pamoja na kuongezeka kwa magonjwa ya kuhara na maambukizo ya kupumua.

Tayari kuna takriban wagonjwa milioni 1 wa kupumua, wagonjwa 575,000 wa magonjwa ya kuhara, na zaidi ya wagonjwa 100,000 wa homa ya manjano ambao wamerekodiwa tangu 7 Oktoba 2023.

Miji muhimu inalengwa katika kuhamisha watu

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu jioni, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada, OCHA, ilisema kuwa zaidi ya watu 200,000 huko Gaza – sawa na asilimia tisa ya watu - wamelazimika kuyahama makazi yao kwa amri zinazotolewa naa Israel za watu kutakiwa kuhama.

Maagizo yaliyotolewa na mamlaka ya Israel siku ya Jumamosi na Jumapili yaliathiri Rafah, Khan Younis na Deir Al-Balah "ambapo jumla ya watu 56,000 walikuwa wamejihifadhi", OCHA ilisema, kabla ya kuonya kwamba mambo haya yanakuja "wakati ambapo maji, usafi wa mazingira na kujisafi vinazidi kumomonyoka huko Gaza, huku magonjwa ya kuambukiza yakiongezeka”.