Skip to main content

COVID-19 ni uthibitisho tosha wa jinsi magonjwa yanavyoweza kulipuka haraka na kuiacha hoi dunia:Guterres

Shirika la Afya Ulimwenguni linafuatilia lahaja mpya ya kirusi cha  corona
Unsplash/Fusion Medical Animation
Shirika la Afya Ulimwenguni linafuatilia lahaja mpya ya kirusi cha corona

COVID-19 ni uthibitisho tosha wa jinsi magonjwa yanavyoweza kulipuka haraka na kuiacha hoi dunia:Guterres

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la COVID-19 limedhihirisha ni jinsi gani magonjwa ya kuambukiza yanavyoweza kuzuka haraka na kusambaa kote duniani, kutoa shinikizo kubwa kwenye mifumo ya afya na kupindua maisha ya watu kwa binadamu wote. 

Kupitia ujumbe wake maalum wa siku ya kimataifa ya maandalizi ya dharura ya magonjwa ya mlipuko inayoadhimishwa tarehe 27 Desemba ya kila mwaka amesema “Janga hilo pia limeonesha kushindwa kwetu kujifunza kutokana na dharura za kiafya kama vile SARS, mafua ya avian, Zika, Ebola na milipuko mingine.” 

Katibu Mkuu ameongeza kuwa COVID-19 pia ni kumbusho kwamba dunia bado haijajiandaa kukomesha milipuko katika jamii na kuizuia isisambae nje ya mipaka na kusababisha janga la kimataifa. 

Amesisistiza kuwa “COVID-19 haitokuwa janga la mwisho kuwakabili duniani. Magonjwa ya kuambukiza yanasalia kuwepo na kusababisha hatari kubwa kwa kila nchi. Wakati huu tukikabiliana na mgogoro wa sasa wa kiafya tunahitaji kujiandaa kwa ajili ya mwingine utakaokuja.” 
 
Bwana Guterres amesema hii inamaanisha kuongeza uwekezaji katika ufuatiliaji maalum, kubaini mapema na kuchukua hatua haraka kukabiliana na mlipuko wowote katika kila nchi na hasa zile zisizojiweza na zilizo hatarini zaidi. 

Pia amesema hii inamaanisha ni kuimarisha huduma za afya za msingi katika ngazi jamii na kuzuia kusambaratika kwa mifumo ya afya. 

Mbali ya hayo ameongeza kuwa “Hii inamaanisha kuhakikisha usawa katika fursa za hatua za kuokoa maisha kama vile chanjo kwa watu wote na pia inamaanisha kufikia lengo la huduma za afya kwa wote.”

Na zaidi ya hapo Guterres amesema hii inamaanisha kujenga mshikamano wa kimataifa kuipa kila nchi fursa ya kukomesha magonjwa ya kuambukiza katika mizizi yake. 

“Mlipuko wa magonjwa popote pale ni uwezekano wa janga la maambukizi kila mahali.Hivyo katika siku hii ya kimataifa ya maadanlizi ya dharura ya milipuko ya magonjwa , hebu tulipe suala hili uzito na uwekezaji unaostahili.”