Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkasa mwingine wa ajali ya meli Atlantiki wadhihirisha hali ya kukata tamaa kwa waathiriwa: UNHCR/IOM

Boti zinazotumiwa na wasafirishaji haramu kwenye njia ya uhamiaji ya Mashariki na Pembe ya Afrika kuelekea Yemen, mojawapo ya njia hatari zaidi duniani.
© IOM/Djibouti
Boti zinazotumiwa na wasafirishaji haramu kwenye njia ya uhamiaji ya Mashariki na Pembe ya Afrika kuelekea Yemen, mojawapo ya njia hatari zaidi duniani.

Mkasa mwingine wa ajali ya meli Atlantiki wadhihirisha hali ya kukata tamaa kwa waathiriwa: UNHCR/IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Habari za mkasa mwingine wa ajali ya meli katika ufuo wa Mauritania ni dalili tosha ya watu waliokata tamaa wanaoendelea kukabiliwa na hali hiyo wanapojaribu kukimbia mapigano, limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Kauli ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa yinafuatia ripoti siku ya Jumatatu wiki hii kwamba makumi ya watu hawajulikani walipo baada ya boti iliyokuwa imebeba mamia ya watu kupinduka kwenye maji kwenye pwani ya mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott.

Miezi ya hivi karibuni imeendelea kushuhudia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaochukua safari za hatari kutoka nchi za kaskazini na magharibi mwa Afrika zikiwemo Senegal, Mauritania na Morocco mwisho wa safari yao mara nyingi ni katika visiwa vya Canary.

"UNHCR, limehuzunishwa sana na ajali hii mbaya ya meli ambayo imesababisha vifo na kupotea kwa watu wengi katika pwani ya Mauritania," amesema  msemaji wa shirika  hilo Shabia Mantoo akiongeza kuwa "Meli hiyo, iliyokuwa ikifuata njia ya Atlantiki ya Magharibi, ilipinduka karibu na Nouakchott, ikigharimu maisha ya takriban watu 15 huku wengine wengi bado hawajulikani walipo."

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM, takriban watu 300 wakiwemo wanawake na watoto walipanda boti hiyo ya mbao ya pirogue nchini Gambia, wakitumia siku saba baharini kabla ya janga hilo kutokea.

Bi. Mantoo amebainisha kuwa hii ilikuwa ajali ya pili mbaya ya meli katika eneo hilo kuripotiwa mwezi huu, baada ya moja kutokea mwanzoni mwa Julai.

Wahamiaji wakiwa wamelala chini ya boti ufukweni Obock Djibout
IOM/Alexander Bee
Wahamiaji wakiwa wamelala chini ya boti ufukweni Obock Djibout

Hatari zinazosababisha mauti

Njia inayoitwa "Njia ya Atlantiki ya Magharibi katika pwani ya Afrika Magharibi ni moja ya njia hatari zaidi duniani, na maelfu ya wahamiaji na wakimbizi wamekuwa  wakizama katika miaka ya hivi karibuni", amesema afisa huyo wa UNHCR akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva Uswisi.

Tangu Juni mwaka jana, zaidi ya boti 76 zilizo na takriban manusura 6,130 zimetia nanga nchini Mauritania, huku karibu 190 ziliangamia baharini kabla ya misiba miwili ya hivi karibuni.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa UNHCR nchini Mauritania, Elizabeth Eyster, wamesisitiza wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono suluhu za kisheria kwa watu walio katika hatari au katika hali mbaya ili waweze kuzunguka nchi na mabara bila kuhatarisha maisha yao, kama inavyozidi kuwa hivi sasa .

"Tunaona matukio ya harakati hizi kuchukuliwa na watu ambao wako katika mazingira magumu sana, wamechoka na kukata tamaa na udhaifu wao wakati mwingine unanyonywa na wasafirishaji haramu wa binadamu kwa njia ya magendo, na wengine," amesema Bi. Mantoo.

Ameongeza kuwa "Kwa hivyo, kuna aina mbalimbali za mbinu ambazo zinatumika, lakini kwa kweli ninazungumzia kukata tamaa kwa watu wanaotumia safari hizi kwa sababu kuna kile wanachokiona kuwa hakuna njia nyingine salama."

Ameendelea kusema kuwa “Tunaomba hatua zichukuliwe kushughulikia hili kwani kumekuwa na majanga mengi katika eneo hili na mengine baharini na nchi kavu. Lakini kunapaswa kuwa na uwajibikaji kwa kweli, kwa mtu yeyote ambaye atafaidika na kukata tamaa kwa watu wengine.”

Wasaka hifadhi wakiokolea na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea
Frontex/Francesco Malavolta
Wasaka hifadhi wakiokolea na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea

Wahamiaji waliopotea wanafuatiliwa

Kwa mujibu wa IOM kuanzia tarehe 1 Januari hadi 15 Julai 2024 pekee, zaidi ya wahamiaji 19,700 waliwasili kwa njia isiyo ya kawaida katika Visiwa vya Canary kwa kutumia njia hii ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023, ambapo wahamiaji 7,590 walirekodiwa, na hilo ni ongezeko la asilimia 160.

Mradi wa Wahamiaji Waliopotea wa IOM umerekodi zaidi ya vifo 4,500 na watu waliopotea kwenye njia hii tangu 2014, ikiwa ni pamoja na vifo vya zaidi ya watu 950 mwaka jana, ambayo ni idadi ya pili kubwa kurekodiwa kwa vifo vya wahamiaji.