Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangladesh: Kamishna Türk alaani msako dhidi ya waandamanaji ataka sheria zizingatiwe 

Mitaa ya Dhaka, Bangladesh.
Austin Curtis/Unsplash
Mitaa ya Dhaka, Bangladesh.

Bangladesh: Kamishna Türk alaani msako dhidi ya waandamanaji ataka sheria zizingatiwe 

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk  hii leo ameitaka serikali ya Bangladesh haraka iweke wazi na kwa kina maelezo kuhusu msako wa wiki iliyopita dhidi ya waandamanaji wakati huu ambapo kuna taarifa za kutishi kuhusu ghasia na wakati huo huo ihakikishe vyombo vya usalama vinazingatia sheria na maadili ya kimataifa ya haki za binadamu.

Taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi na Ofisi ya Kamisha huyo imemnukuu akisema ripoti za awali zinadokeza kuwa zaidi ya watu 170 wameuawa na zaidi ya 1000 wamejerhiwa, baadhi yao wakinyimwa huduma za matibabu. “Wengine wengi hawajulikani waliko kufuatia maandamano ya wanafunzi na vikundi vya vijana dhidi ya sera za serikali.”

Tweet URL

Amesema waandishi wa habari wawili wameripotiwa kuuawa na makumi kadhaa wamejeruhiwa. Mamia ya watu wamekamatwa, wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu wa upinzani, amesema Kamishna Türk.

Itakuwa ni vema serikali ikitoa taarifa za kina kuhusu waliouawa, waliojeruhiwa au wanaoshikiliwa korokoroni kwa maslahi ya familia zao.”

Ametaka pia serikali irejeshe bila kuchelewa mtandao wa intaneti ili kuruhusu wananchi wakiwemo waandishi wa habari na vyombo vya habari kuwasiliana bila vikwazo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Kamishna Türk  amesema ni muhimu kwa serikali kuerejesha imani ya wananchi na kujenga mazingira bora ya mazungumza na umma katika masuala yaliyosababisha kuanza kwa maandamano tarehe Mosi mwezi huu wa Julai.

Chanzo cha maandamano

Tangu tarehe 1 mwezi huu wa Julai, wanafunzi nchini kote Bangladesh wamekuwa wakiandamana dhidi ya hatua ya serikali ya kurejesha mfumo wa kiwango cha ajira za serikali kwa misingi ya makundi fulani, hatua ambayo wanafunzi wanasema ni upendeleo wakati huu ambapo ajira ni shida nchini humo.

Ghasia ziliibuka tarehe 15 Julai baada ya kauli za uchochezi kwa umma kutoka kwa viongozi wa serikali na vijana wenye mrengo na serikali kushambulia waandamanaji.Baadhi ya waandamanaji walijibu vitendo hivyo kwa kuchoma moto mali za umma yakiwemo magari.

Tarehe 18 Julai serikali ilitangaza hali ya hatari nchi nzima na kutaka jeshi lirejeshe utulivu na utawala wa sheria huku ikipatia mamlaka jeshi kujibu mashambulizi kwa risasi.

Matumaini ya Türk  

Bwana Türk  amesema ni matumaini yake kuwa uamuzi wa Jumapili iliyopita wa Mahakama Kuu ya kupunguza kidogo kiwango cha mgao wa ajira za serikali unaweza kufungua fursa ya kujenga imani kwa umma na mashauriano jumuishi nay a wazi juu ya hoja husika.

Ametaka pia serikali ifanye uchunguzi huru, wazi na wa kina juu ya madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu, huku akisema “Ofisi yangu iko tayari kusaidia serikali katika suala hilo.”

Wakati huo huo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu wameitaka serikali ya Bangladesh iache mara moja msako dhidi ya waandamanaji na wapinzaji wa kisiasa, irejeshe mtandao wa intaneti na iwajibike na ukiukwaji wa haki za binadamu.