Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UN aeleza wasiwasi wake juu ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Yemen, na hatari ya mzozo wa kikanda

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (Maktaba)
UN Tajikistan/Didor Sadulloev
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (Maktaba)

Mkuu wa UN aeleza wasiwasi wake juu ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Yemen, na hatari ya mzozo wa kikanda

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumzia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel dhidi ya Yemen katika mji wake wa bandari wa Hudaydah, ambayo inaripotiwa kuwaua takriban watu sita na kujeruhi zaidi ya 80, kwa kutoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mzozo huo "kujizuia".

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu Guterres alibainisha kuwa Israel ilidai kuhusika na mashambulizi hayo, ambayo yalifanyika hapo jana Jumamosi, kama jibu la mashambulizi ya hapo awali dhidi ya Israel yaliyofanywa na Wahouthi (waliojulikana rasmi kama Ansar Allah) kundi ambalo linadhibiti maeneo mengi ya Yemen akiwemo Hudaydah.

Mashambulizi hayo yametokea baada ya shambulizi la ndege zisizo na rubani katika mji wa Tel Aviv nchini Israel siku ya Ijumaa kuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine 10. Shambulio hilo lilidaiwa kutekelezwa na Wahouthi na kupelekea waziri mkuu wa Serikali ya Israel kuapa Kujibu mashambulizi.

Mashambulizi yaliyofanywa na Waisrael siku ya Jumamosi yaligonga miundombinu ya umeme na kiwanda cha kusafisha mafuta, na kusababisha moto mkubwa.

Juhudi za upatanishi kati ya Wahouthi na serikali ya Yemen zimekwama katika miezi ya hivi karibuni, kufuatia kuanza kwa vita huko Gaza mwezi Oktoba, Wahouthi waliahidi kushambulia kile walichokiona kuwa maslahi ya meli ya Israel katika pwani ya Bahari Nyekundu, kama njia mojawapo ya kuonesha mshikamano na Wapalestina wanaoshambuliwa na jeshi la Israel huko Ukanda wa Gaza.

Kwa upande mwingine, muungano unaoongozwa na Marekani (Marekani) unaotetea meli katika Bahari Nyekundu umeendelea kushambulia maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi huko Hudaydah, mji mkuu Sana'a na Ta'iz.

Waasi wa Houthi wameripotiwa kuonya kwamba jibu la kundi hilo kwa mashambulizi ya anga ya Israel "litakuwa kubwa" na kwamba kundi hilo litaendelea kushambulia Israel na kwamba hakutakuwa na "mistari nyekundu".

Mzozo wa Yemen ulioanza mwaka 2015 umekuwa mbaya kwa raia. Umoja wa Mataifa unasema vita hivyo vimeharibu sekta nyingi nchini Yemen, ikiwa ni pamoja na huduma za afya, na kusababisha mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

Karibu nusu ya idadi ya watu, ambao ni takriban watu milioni 18.2, wanahitaji aina fulani ya usaidizi.