Mauaji ya Gaza leo lazima yachunguzwe: Guterres

30 Machi 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru na wa wazi dhidi ya machafuko yaliyozuka leo Ijumaa kwenye uzio wa Gaza kati ya Wapalestina waliokuwa wakishiriki maandamano na vikosi vya ulinzi vya Israel na kusababisha vifo vya watu 15 na wengine wengi kujeruhiwa.

Wito huo wa uchunguzi umekuja wakati baraza la usalama linafanya kikao cha dharura ili wajumbe wapewe taarifa kuhusu tukio hilo.
Maelfu ya wapalestina wameaandamana leo Gaza kwenye mpaka na Israel kupinga vikwazo vya muda mrefu dhidi ya ukanda huo.

Afisa wa Umoja wa Mataifa amesema wizara ya afya ya Palestina imethibitisha kwamba wapalestina 15 wameuawa na wengine zaidi ya 1000 kujeruhiwa ikiwemo kwa kukosa hewa sababu ya mabomu ya michozi.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Guterres amesema amesikitishwa sana na tukio la leona anatiwa hofu hivyo ameziomba pande husika kujizuia na vitendo vyovyote ambavyo vitasababisha majeruhi au vifo zaidi hususan kwa raia.

Amesisitiza kuwa zahma kama hii inadhihirisha haja ya haraka wa kufufua mchakato wa amani wenye lengo la kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya majadiliano ya kupata suluhu ya mzozo wa Mashariki ya Kati kwa njia ya amani ambayo itaruhusu Wapalestina na waisrael kuishi pamoja kwa amani na usalama na kusema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia mchakato huo
 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter